Haaland aomba radhi kipigo Man City
Muktasari:
- Nyota huyo wa Norway mwenye umri wa miaka 25 alikuwa na usiku wa kusahaulika, huku kurejea kwake nyumbani nchini Norway kukigeuka kuwa jinamizi na kuiacha Man City katika hatari ya kukosa kufuzu moja kwa moja hatua ya mtoano ya michuano hiyo baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1.
MANCHESTER, ENGLAND: STRAIKA wa Manchester City, Erling Haaland amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo baada ya kupoteza kwa aibu kwenye Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu ndogo ya Bodoe/Glimt usiku wa Jumanne.
Nyota huyo wa Norway mwenye umri wa miaka 25 alikuwa na usiku wa kusahaulika, huku kurejea kwake nyumbani nchini Norway kukigeuka kuwa jinamizi na kuiacha Man City katika hatari ya kukosa kufuzu moja kwa moja hatua ya mtoano ya michuano hiyo baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1.
Kocha Pep Guardiola alikiri baada ya kipigo hicho aliposema: “Hisia ni kwamba kila kitu kinaenda vibaya,” baada ya kushuhudia moja ya mshangao mkubwa zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Fedheha hiyo ilitokea kwenye joto la nyuzi -9°C, siku chache tu baada ya Man City kupata kipigo kingine cha aibu kwenye dabi ya Manchester walipochapwa mabao 2-0 na Manchester United uwanjani Old Trafford, Jumamosi iliyopita.
Haaland, ambaye alikiri kuwa kiwango cha timu hakikuwa cha kuridhisha, aliongeza mfululizo wake mbaya wa kutofunga, akiwa na bao moja tu penalti dhidi ya Brighton katika mechi zake nane za mwisho ni moja ya sababu muhimu za chama hilo kukumbana na matokeo mabovu.
Haaland alisema: “Ni aibu. Nachukua jukumu lote kwa kushindwa kufunga. Naomba radhi kwa kila mtu, kila shabiki wa Man City aliyesafiri kuja kutuunga mkono. Kwa kweli ni aibu. Sijui niseme nini kingine kwa sababu sina majibu na ninachoweza kusema ni samahani. Ushindi ulikuwa wa haki na kile tulichokionyesha hakitoshi. Wanacheza kwa kiwango cha juu wanapokuwa nyumbani. Tulicheza vizuri hadi walitupofunga bao la kwanza, lakini wakafunga tena. Kisha Jens (Petter Hauge) akafunga bao la mwaka. Tulijaribu kadri tulivyoweza, lakini kuna kitu kinakosekana.”