Bosi Madrid ampigia hesabu kali Haaland
Muktasari:
- Perez anataka kumsajili nyota wa Manchester City, Erling Haaland, majira yajayo ya joto, na pia amemjumuisha aliyekuwa kocha wa Chelsea, Enzo Maresca kwenye orodha ya makocha wa kuinoa miamba hiyo.
MADRID, HISPANIA: RAIS wa Real Madrid, Florentino Perez, anaangalia uwezekano wa kufanya usajili mkubwa ili kuwainua mabingwa hao wa Hispania kutoka kwenye kuyumba.
Perez anataka kumsajili nyota wa Manchester City, Erling Haaland, majira yajayo ya joto, na pia amemjumuisha aliyekuwa kocha wa Chelsea, Enzo Maresca kwenye orodha ya makocha wa kuinoa miamba hiyo.
Mfanyabiashara huyo wa Kihispaniola bado ana mawasiliano ya karibu na wakala wa Haaland, Rafaela Pimenta, na anatumaini kufanya hatua rasmi wakati wa majira ya kiangazi ya mwaka huu.
Hata kabla ya nyota huyo wa Norway kuhamia Manchester City mwaka 2022, Madrid waliwasilisha ofa lakini Haaland alichagua kufanya kazi chini ya kocha Pep Guardiola. Haaland anajulikana kuwa mpenzi mkubwa wa Hispania na anaiona Real Madrid kama kilele cha mafanikio katika taaluma yake ya soka.
Hata hivyo, dili hilo halitakuwa rahisi kutokana na mkataba mkubwa wa Haaland unaomfunga Man City hadi mwaka 2034.
Real Madrid italazimika kutoa ada kubwa ya zaidi ya Euro 500 milioni, jambo litakalowalazimu kuridhia kumuuzia winga wa Kibrazili Vinicius Junior.
Perez ana matumaini kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa mapema majira ya joto, lakini kuna maswali kuhusu uwezekano wa utekelezaji wa dili ambalo lingeweka rekodi mpya ya usajili duniani.
Kwa sasa, Real Madrid ipo nyuma ya vinara wa La Liga, Barcelona, kwa pointi nne katikati ya msimu. Xabi Alonso alifukuzwa kazi baada ya kipigo cha mabao 3–2 kutoka kwa wapinzani wao wakubwa kwenye fainali ya Super Cup ya Hispania, kabla ya Alvaro Arbeloa kuchukua nafasi kwa muda.
Maresca anaonekana kuwa chaguo la kweli zaidi la kudumu majira ya joto. Jina la Jurgen Klopp pia limejadiliwa ndani ya klabu, lakini aliyekuwa kocha wa Liverpool bado amefungwa kwa muda mrefu na mtandao wa Red Bull kama mkurugenzi wao wa michezo duniani.
Zinedine Zidane pia ni miongoni mwa wagombea wanaopendelewa, lakini ana uwezekano mkubwa wa kuchukua nafasi ya ukocha wa timu ya taifa ya Ufaransa baada ya Kombe la Dunia 2026. Mshindi huyo mara tatu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya pia ana uhusiano usio mzuri na Perez huko Los Blancos.