Kigogo Man United atua Italia dili la Osimhen

Muktasari:
- Osimhen ni mmoja wa wachezaji wanaowindwa zaidi Ulaya na Man United imetuma mmoja wa wataalamu wake wa usajili kujaribu kumshawishi Osimhen pamoja na Napoli ili nyota huyo akubali kujiunga na timu hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: RIPOTI zimefichua kuwa wawakilishi wa Manchester United wamesafiri kwenda Italia kwa ajili ya kuzungumza na Napoli kuhusu uwezekano wa kuipata huduma ya straika wa timu hiyo na Nigeria, Victor Osimhen kwa mabadilishano ya wachezaji na kiasi cha pesa.
Inaelezwa Man United iko tayari kumtoa straika Rasmus Hojlund pamoja na kiasi cha pesa ili kumpata nyota huyo wa Nigeria.
Osimhen ni mmoja wa wachezaji wanaowindwa zaidi Ulaya na Man United imetuma mmoja wa wataalamu wake wa usajili kujaribu kumshawishi Osimhen pamoja na Napoli ili nyota huyo akubali kujiunga na timu hiyo.
Mkuu wa masuala ya usajili wa Man United, Matt Hargreaves amewasili Italia kuzungumza na rais wa Napoli Aurelio Di Laurentiis na mkurugenzi wa michezo Giovanni Manna.
Napoli wako tayari kumruhusu Osimhen kujiunga na Man United lakini wanahitaji Pauni 33.5 milioni na pamoja na Hojlund.
Osimhen anatarajiwa kurudi Naples siku chache zijazo, baada ya kuwa kwa mkopo wa msimu mmoja na Galatasaray, ambako amefunga mabao 36 na kushinda taji la ligi.
Napoli walishinda taji la Serie A bila yeye wikiendi hii chini ya kocha Antonio Conte, ikiwa ni miaka miwili tu baada ya yeye kuwaletea taji hilo kwa mabao 31 katika mashindano yote aliyofunga mwaka 2023.
Licha ya ofa hiyo kutoka kwa Man United, ripoti kutoka Sky Sports zinaeleza kwamba Osimhen yupo katika mazungumzo na Al-Hilal ya Saudi Arabia ambayo inatamani kumnasa katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo inataka akazibe pengo la Neymar Jr aliyerudi Brazil.