Kevin De bruyne, Marekani ipo hivi

Muktasari:
- Nahodha huyo wa Manchester City, mwenye umri wa miaka 33, hadi sasa hajafikia mwafaka juu ya kuurefusha mkataba wake na timu hiyo na ripoti zinaeleza amepata ofa nono Saudi Arabia lakini mwenyewe anatamani kutua Marekani.
CALIFORNIA,MAREKANI: KIUNGO wa Manchester City Kevin de Bruyne ameripotiwa kuzungumza na San Diego ya Marekani juu ya uwezekano wa kujiunga nayo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi pale mkataba wake utakapomalizika.
Nahodha huyo wa Manchester City, mwenye umri wa miaka 33, hadi sasa hajafikia mwafaka juu ya kuurefusha mkataba wake na timu hiyo na ripoti zinaeleza amepata ofa nono Saudi Arabia lakini mwenyewe anatamani kutua Marekani.
San Diego, ambayo ni kati ya timu changa katika ligi ya MLS, imefanya mazungumzo na wawakilishi wake juu ya kuona kama wana-weza kumpata Mbelgiji huyu lakini hadi sasa hakuna mwafaka uliofikiwa.
Mwafaka umeshindwa kufikiwa kwa sababu mahitaji ya mshahara ya De Bruyne yanasemekana kuwa ni makubwa zaidi tofauti na bajeti ya timu hiyo.
Tyler Heaps, ambaye ni mkurugenzi wa michezo wa San Diego, alikanusha taarifa za kwamba wamefikia mwafaka ingawa alikiri mazungumzo yamefanyika.
“Hizo habari, sijui zinatoka wapi. Nilizungumza na wakala, De Bruyne ni mchezaji mzuri sana na anapenda mazingira ya Jiji la San Diego. Huwa anapumzika hapa kila mwaka, nimezungumza naye, lakini nitakwambia kitu, mshahara anaohitaji hauendani na bajeti yetu kwa sasa.”
Kevin de Bruyne amecheza mechi 280 za Ligi Kuu England amefunga mabao 70 na kutoa asisti za mabao mengine 118.
Staa huyo alitumia muda mwingi wa msimu huu akiwa nje ya uwanja kutokana na majeraha.