Jude amtibua Thomas Tuchel, ampa makavu yake
Muktasari:
- Tuchel ametoa kauli hiyo kwa kumlenga Bellingham, baada ya kiungo huyo kuonyesha kukerwa na kitendo cha kutolewa uwanjani dakika za mwisho katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Albania jana Jumapili, Novemba 16, 2025.
Kocha wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel amemtaka kiungo Jude Bellingham kuheshimu uamuzi wa benchi la ufundi, ili kuleta mazingira chanya ya ushirikiano ambayo yataendelea kuleta furaha baina yao.
Tuchel ametoa kauli hiyo kwa kumlenga Bellingham, baada ya kiungo huyo kuonyesha kukerwa na kitendo cha kutolewa uwanjani dakika za mwisho katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Albania jana Jumapili, Novemba 16, 2025.
Bao mbili za Harry Kane ziliipa England ushindi wa 2-0 mjini Tirana, ulioifanya makamu bingwa wa Euro 2024 kukamilisha kampeni bora kabisa ya Kundi K kwa ushindi wa mechi nane na kutoruhusu bao lolote.
Bellingham alikuwa miongoni mwa wachezaji saba waliobadilishwa kutoka kikosi kilichoshinda dhidi ya Serbia siku ya Alhamisi, na alitolewa dakika sita kabla ya mechi kumalizika katika mechi yake ya kwanza kuanza akiwa na England tangu Juni 2025.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, alionyesha kukasirika kwa kuinua mikono baada ya bao la pili, huku akiona Morgan Rogers akijiandaa kuchukua nafasi yake kitendo ambacho Tuchel hakukifurahia.
“Uamuzi wa benchi la ufundi lazima uheshimiwe, na lazima mchezaji aukubali. Haiwezekani mchezaji mwenzako anakusubiri pembeni ya uwanja halafu wewe muhusika unaendelea kulalamika, ni lazima ukubali uamuzi uliofanywa, uuheshimu, na aendelee kufanya hivyo,” amesema kocha huyo raia wa Ujerumani.
Alipoulizwa kama kauli hiyo ilimuhusu Bellingham, kocha huyo amesema inawezekana ikawa hivyo lakini wachezaji wake wote wanatakiwa kuwa na heshima kwa chochote kitakachoamuliwa.
“Inamuhusu huyo unayemzungumzia hapa, lakini pia inawahusu wachezaji wengine ambao huenda wakawa na tabia kama hiyo, hii ni timu yetu sote na sio timu ya mtu mmoja, tunapaswa ksuhirikiana kwa umoja ili kupata matokeo chanya.
“Nimeona tu Bellingham hakufurahi. Sitaki kulifanya kuwa jambo kubwa zaidi kwa sasa. Nadhani kwa kiwango fulani ukiwa na wachezaji kama Jude, ambao ni washindani kupita kiasi, hawatapenda kamwe kutolewa, lakini kama ulivyosema, neno langu linasimama kama nilivyomaanisha.
“Haya ni kuhusu viwango na ubora, na ni ahadi na heshima kwa kila mmoja, hivyo mtu anasubiri nje, na hatutabadilisha uamuzi kwa sababu mtu analalamika kwa uamuzi tulioufanya,” amesema Tuchel.
Imekuwa mwaka wa kwanza wenye mafanikio kwa kocha huyo Mjerumani, ambaye atawafahamu wapinzani wa England wakati wa droo ya Desemba 5, 2025 baada ya kuwa timu ya kwanza ya Ulaya kucheza angalau mechi sita za kufuzu na kushinda zote bila kuruhusu bao.