Joshua afunguka kwa mara ya kwanza
Muktasari:
- Joshua, ambaye alikuwa abiria katika siti ya nyuma, alilazwa hospitalini baada ya kupata majeraha ambayo awali yaliripotiwa kuwa madogo, katika ajali iliyotokea wakati gari alilokuwa akisafiria lilipogonga lori lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara.
LONDON, ENGLAND: BONDIA raia wa England, Anthony Joshua ameposti kwenye mitandao ya kijamii kwa mara ya kwanza tangu alipopata ajali ya gari iliyoua marafiki wake wawili wa karibu nchini Nigeria.
Joshua, ambaye alikuwa abiria katika siti ya nyuma, alilazwa hospitalini baada ya kupata majeraha ambayo awali yaliripotiwa kuwa madogo, katika ajali iliyotokea wakati gari alilokuwa akisafiria lilipogonga lori lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara.
Ajali hiyo iliyotokea Jumatatu asubuhi kwenye barabara kuu ya Jimbo la Ogun, ilishika vichwa vya habari duniani kwa takribani siku tatu.
Dereva aliyekuwa anaendesha gari aliyopanda Joshua, Adeniyi Mobolaji Kayode, mwenye umri wa miaka 46, alishtakiwa mahakamani kwa kusababisha vifo kwa kuendesha gari bila ya kuwa makini wala kuchukua tahadhari ya kutosha.
Vilevile dereva huyo alishtakiwa kwa kuendesha gari bila leseni halali.
Hata hivyo, Kayode amekanusha mashtaka yote dhidi yake na kwa mujibu wa mawakili wake, anadai kwamba ajali hiyo ilikuwa ajali tu kama ajali nyingine na changamoto kubwa ni kwamba breki hazikufanya kazi.
Hadi sasa kuna taarifa mchanganyiko kuhusu hali halisi ya majeraha ya Joshua, lakini mshindi huyo wa mara mbili wa ubingwa wa juu wa dunia mwenye umri wa miaka 36 kwa sasa yupo nchi ya England baada ya kutoka hospitalini siku ya Sikukuu ya Mwaka Mpya.
Joshua ameandika kwenye mitandao ya kijamii kwa mara ya kwanza jana tangu ajali hiyo ilipotokea.
Katika picha moja iliyopostiwa Instagram, Joshua alionekana akiwa ameketi kwenye kochi akiwa na watu wanne wengine, mmoja akiwa ameshika picha iliyowekwa kwenye fremu.
Pamoja na picha hizo, Joshua aliweka maandishi mafupi yenye maneno matatu: “My Brothers Keeper” (Mlinzi wa Ndugu Zangu).
Kiongozi mmoja wa familia aliiambia BBC kwamba Joshua alikuwa akisafiri kwenda Sagamu kutembelea jamaa kwa ajili ya sherehe za Mwaka Mpya.