Antony Joshua adaiwa kustaafu ngumi
Muktasari:
- Joshua, mwenye umri wa miaka 36, alipata majeraha madogo baada ya gari aina ya Lexus SUV alilokuwa akisafiria kugonga lori lililokuwa limesimama pembeni ya barabara huko Lagos, Desemba 29.
LONDON, ENGLAND: NDUGU wa Anthony Joshua anaripotiwa kufichua kuwa bondia huyo ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia wa uzito wa juu mara mbili amestaafu rasmi ngumi baada ya ajali ya gari iliyosababisha vifo vya rafiki zake wawili nchini Nigeria.
Joshua, mwenye umri wa miaka 36, alipata majeraha madogo baada ya gari aina ya Lexus SUV alilokuwa akisafiria kugonga lori lililokuwa limesimama pembeni ya barabara huko Lagos, Desemba 29.
Bondia huyo mzaliwa wa Watford, ambaye alikuwa nchini humo kuwatembelea ndugu zake, aliwahishwa hospitalini kabla ya kurejea England wiki iliyopita.
Sina Ghami na Latif ‘Latz’ Ayodele, ambao ni marafiki wa karibu wa bondia huyo, wote walifariki dunia katika ajali hiyo.
Adeniyi Mobolaji Kayode, ambaye ndio alikuwa dereva wa gari wakati ajali inatokea, alifikishwa mahakamani akishtakiwa kwa kosa la kusababisha vifo kwa kuendesha gari bila ya kuwa makini, kuendesha bila leseni na uendeshaji wa hatari.
Hata hivyo, Kayode mwenye umri wa miaka 46, aliachiwa kwa dhamana ya Naira 5,000,000 na kesi yake itasikilizwa tena Januari 20.
Joshua alivunja ukimya wake Jumapili ya wiki iliyopita akiweka chapisho katika ukurasa wake wa Instagram kwa mara ya kwanza tangu apatwe na ajali.
Bondia huyo alichapisha picha mbili, moja ikimuonyesha akiwa pamoja na wanafamilia wa Ghami na Ayodele.
Ajali hiyo ilitokea siku 10 tu baada ya Joshua kumpiga kwa KO Jake Paul huko Miami.
Inaelezwa kwa sasa, ndondi huenda si kipaumbele kwa Joshua kutokana na msiba wa kupoteza marafiki zake wawili, lakini kwa mujibu wa mwanafamilia, Joshua tayari ameshastaafu.
Akizungumza na gazeti la Punch, mjomba wa Joshua, Adedamola, amesema bondia huyo wa uzito wa juu amestaafu ndondi na sababu kubwa ni ajali hiyo.
“Ametuambia kuwa amestaafu na hilo ndilo jambo ambalo sisi kama ndugu linatufurahisha, kwa sababu kila anapopigana ulingoni sisi huwa tunaguswa sana kihisia, pale anapopoteza pambano mioyo huwa inaumia sana. Huwa ni mateso makubwa kwetu. Alipotuambia kwamba anaachana na ngumi tulifurahi.”
Ikiwa Joshua atatangaza hadharani kustaafu rasmi, ataingia kwenye historia kama mmoja wa mabondia wa uzito wa juu waliofanikiwa zaidi nchini England.
Awali, alikuwa akihusishwa na pambano dhidi ya raia mwenzake wa England Tyson Fury, ambaye hivi karibuni alitangaza kurejea kutoka kustaafu.