Jezi Namba 10 yamlevya Cunha
Muktasari:
- Mbrazili huyo alithibitishwa rasmi Namba 10 mpya wa Man United, Jumanne iliyopita baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea Wolves kwa ada ya uhamisho ya Pauni 62.5 milioni.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA mpya wa Manchester United, Matheus Cunha amefichua alibadilishana jezi na Marcus Rashford ili kuwa na jezi Namba 10 ya timu hiyo nyumbani siku kadhaa kabla ya kutua Old Trafford na kukabidhiwa namba hiyo.
Mbrazili huyo alithibitishwa rasmi Namba 10 mpya wa Man United, Jumanne iliyopita baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea Wolves kwa ada ya uhamisho ya Pauni 62.5 milioni.
Rashford alikabidhiwa jezi huyo wakati Zlatan Ibrahimovic alipoondoka kwenye timu msimu wa 2017/18. Lakini, baada ya kutibuna na Kocha Ruben Amorim msimu uliopita, Rashford siku zake kwenye klabu hiyo zimefika ukomo na hivyo kinyang’anywa jezi ambayo imechukuliwa na Cunha.
Cunha, 26, siku zote amekuwa mpenzi mkubwa wa jezi Namba 10 na aliwahi kuvaa namba hiyo alipokuwa Hertha Berlin na Wolves.
Lakini, kwenye mahojiano yake alisema, kuvaa Namba 10 ya Man United kuna heshima kubwa, kutokana na waliomtangulia, akiwamo Rashford.
Alisema: “Siku zote nilikuwa nikiifikiria hii jezi – mtu mmoja ninayemfikiria zaidi ni Wayne Rooney, wakati nakuwa ndiye mtu niliyekuwa nikimtazama akicheza. Kuna wachezaji wengi, Van Nistelrooy, Ibrahimovic. Nilibadilishana jezi pia na Marcus Rashford, ili kuwa na hii jezi nyumbani kwangu.”
Cunha alichangia mabao 21 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita katika mechi 33 alizocheza akiwa na kikosi cha Wolves, jambo ambalo lilimfanya kocha Amorim kunasa saini yake haraka.
Kwenye kikosi cha Man United, wachezaji waliokuwa vinara wa mabao kwenye ligi msimu uliopita ni Amad Diallo na Bruno Fernandes, ambao kila mmoja alifunga mara nane.
Staa Cunha tayari ameshaanza mazoezi kwenye timu yake mpya ya Man United, akisubiri kwa hamu kuanza kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.