Jesus ampa Gyokeres maujanja ya kutoboa
Muktasari:
- Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Brazil amefichua kuwa hafanyi mazungumzo tu na kikosi cha vijana cha Mikel Arteta kuhusu kile kinachohitajika kufika mwisho na kushinda, Jesus amekiri kuwa amekuwa akizungumza na mshambuliaji mwenye wakati mgumu Viktor Gyokeres namna ya kufanya ili kuwa bora.
LONDON, ENGLAND: GABRIEL Jesus ni mmoja wa wachezaji saba tu wa Arsenal wanaojua maana ya kushinda ubingwa. Lakini ndiye pekee aliyewahi kushinda taji la Ligi Kuu England kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Brazil amefichua kuwa hafanyi mazungumzo tu na kikosi cha vijana cha Mikel Arteta kuhusu kile kinachohitajika kufika mwisho na kushinda, Jesus amekiri kuwa amekuwa akizungumza na mshambuliaji mwenye wakati mgumu Viktor Gyokeres namna ya kufanya ili kuwa bora.
Gyokeres bado hajajipata vile inavyopaswa tangu aliponaswa na Arsenal kwenye dirisha la majira ya kiangazi lililopita kwa ada ya Pauni 63.5 milioni.
Huko alikotoka Sporting Lisbon, Gyokeres alikuwa moto kwelikweli kwa kufunga mabao, lakini hali imekuwa tofauti tangu alipotua Arsenal.
Jesus, aliyeshinda mataji manne akiwa na Manchester City, pia anaamini Arsenal bado ni tishio kubwa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya wanapojaribu kuendeleza rekodi yao ya asilimia 100 katika mashindano hayo dhidi ya Inter Milan, iliyotarajia kufanyika usiku wa Jumanne.
Staa huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 45 milioni kutoka Man City mwaka 2022 amesema: “Kwa bahati mbaya, misimu mitatu iliyopita Arsenal tumemaliza nafasi ya pili. Lakini tuko katika hali nzuri, tuna furaha kwa sababu tupo katika nafasi tuliyonayo na kwa ujumla tunashinda michezo hata kama tumetoka sare katika mechi mbili zilizopita."
"Tunazungumzia Ligi Kuu ni ngumu. Je, umeona matokeo ya raundi iliyopita? Kila timu iliyokuwa juu ilipoteza pointi. Hiyo ndiyo Ligi Kuu na mambo kama haya hutokea. Wakati nilipokuwa Man City na kushinda mataji, mara pekee ambayo hatukupoteza pointi nyingi ni pale tulipovuka alama 100. Nawaambia wachezaji hilo.”
Na je, kuhusu Gyokeres? Baada ya kufunga dhidi ya Chelsea, alionekana tena kuhangaika katika sare ya bila kufungana dhidi ya Nottingham Forest Jumamosi iliyopita, na inaonekana Jesus, mwenye umri wa miaka 28, alitarajia kuanza katika mchezo wa San Siro na amesema: “Vik ni mtu mzuri sana. Kwa bahati mbaya alipokuja, sikuwepo kwa sababu nilikuwa nimeumia na nilikuwa nafanya mazoezi ya kurejea uwanjani Brazil nikiwa na familia yangu.”