Jarmila: Rekodi yake ya miaka 37 yazidi kutesa Olimpiki
Muktasari:
- Aliiweka katika mashindano yaliyofanyika Munich, Ujerumani na alikimbia kwa muda wa 1:53.28 na kufuatiwa na Nadezha Olizarenko wa Urusi (1:53.43) na kuwa rekodi ya dunia ya mashindano ya riadha ya mtu mmoja iliyodumu kwa muda mrefu zaidi.
Jarmila kratochvilova ni jina maarufu sana duniani hasa kwenye michezo ya Olimpiki. Kuna rekodi kibao ambazo ziliwekwa miaka ya nyuma lakini ya mwanamama huyu raia wa Jamhuri ya Czech (zamani Czechoslovakia kabla ya Slovakia kujitenga) haijawahi kuvunjwa kwa miaka takriban 37 hadi sasa.
Aliiweka katika mashindano yaliyofanyika Munich, Ujerumani na alikimbia kwa muda wa 1:53.28 na kufuatiwa na Nadezha Olizarenko wa Urusi (1:53.43) na kuwa rekodi ya dunia ya mashindano ya riadha ya mtu mmoja iliyodumu kwa muda mrefu zaidi.
Ni rekodi ya riadha ya mbio za mita 800 na tangu siku ilipowekwa rekodi hiyo, ni wanariadha wawili tu ndio walioikaribia, Pamela Jelimo wa Kenya (2008) na Caster Semenya wa Afrika ya Kusini (2018).
Mwanamama huyu wa Czech aliyeweka rekodi hii akiwa na miaka 32 na sasa ana miaka 66, ni miongoni mwa wanamichezo wastaafu anayeheshimika sana katika nchi yake na anatumia muda mwingi katika kijiji chake kilichopo Jimbo la Bohemia akiwa ni mwalimu wa riadha wa vijana.
Hata hivyo, kwa sasa yupo Ufaransa katika michezo ya Olimpiki akiwa na kikosi cha riadha cha nchi yake akisubiri kuona kama kuna mwanamke atakayeweza kuvunja rekodi yake au itaendelea kudumu.
Hii inatokana na wazo la kuanza na mfumo mpya wa kuweka rekodi za dunia kwa kufuta rekodi zote za riadha zilizowekwa kabla ya mwaka 2005.
Wazo hili linajengwa na hoja ya huenda walioziweka rekodi zisiovunjika kirahisi walitumia dawa za kuongeza nguvu na wakati ule hapakuwepo vipimo vya uhakika wa kugundua ujanja huo.
Rais wa Shririkisho la Kimataifa la Riadha (IAAF), Sebastian Coe ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa Filbert Bayi wa Tanzania katika riadha miaka ya 1970, ni mmoja wa wanariadha wanaounga mkono mpango huo.
Alisema mpango huo ni mzuri na ni vyema kufungua
ukurasa mpya wa rekodi za dunia za mchezo wa riadha.
Akizungumzia wazo hili, Jarmila alisema huo ni upuuzi mtupu na kusisitiza katika maisha yake hajawahi kutumia dawa za kuongeza nguvu na mwendo wake wa kasi ulitokana na mpango mzuri wa mazoezi.
Alisema uamuzi huo ukifanyika basi utakuwa wa kitoto kwa sababu rekodi zinafutwa kwenye makaratasi, lakini hazifutiki kwenye vichwa vya wanamichezo.
Ushindani katika riadha unazidi kuwa mkubwa kila miaka ikipita kutokana na kukua kwa teknolojia kulikosababisha wanariadha kutumia vifaa vya kisasa na viwanja vizuri.
Matokeo yake ni rekodi za dunia zilizoonekana sio rahisi kuvunjwa na kudumu muda mrefu zimefanywa kuwa sehemu ya historia.
Baadhi ya rekodi zilizoonekana hazivunjiki zimevunjwa mara mbili, tatu au zaidi katika miaka ya karibuni. Lakini hii ya mwanamama huyu inaonekana kama kujaribu kuvunja jabali kwa kutumia mikono.
Kratochviola anaendelea kuishi katika kijiji alichozaliwa cha Golcuv Jenikov. Akiwa mdogo alifanya kazi katika shamba la mjomba wake, hasa wakati wa kuvuna viazi kwa mkono, lakini akipenda riadha.
Alipokuwa na miaka 12 alijitokeza kuwa mmoja wa wakimbiaji wazuri kijijini na katika michezo ya shule.
Wakati akifanya kazi kama mhasibu alikwenda Urusi mwaka 1980 kuiwakilisha nchi yake katika michezo ya Olimpiki baada ya kufanya mazoezi alfajiri na jioni kila siku. Matokeo yake, alishinda medali ya fedha katika mbio za mita 400.
Aliporudi nyumbani akaendelea na mazoezi barabarani, katika njia za shambani na wakati mwengine kwenye theluji.
Kwa mujibu wa mwalimu wake, Miroslav Kvac, Kratochviola alipenda kufanya mazoezi kila wakati na mara nyingine alilazimika kumpumzisha kwa kumfungia chumbani ili alale, lakini hata alipokuwa chumbani alifanya mazoezi ya kunyoosha misuli.
Agosti 10, 1983 aliweka rekodi nyingine ya dunia ya mita 400, akitumia sekunde 47.99, hata hivyo, ilikuja kuvunjwa na Marita Koch akiiwakilisha Ujerumani Mashariki (sasa Ujerumani baada ya Ujerumani Mashariki kuporomoka) akitumia sekunde 47.60. ALifanya hivyo Oktoba 6, 1985 na rekodi hii imesimama hadi sasa.
Swali ni je, rekodi ya mwanamama huyu itavunjwa katika michuano ya Olimpiki inayoendelea Paris, Ufaransa au itaendelea kusimama kama ilivyo. Tusubiri.