Ishu ya Thiery Henry sababu ni hii

Muktasari:
- Henry alikuwa nahodha wa Arsenal wakati huo na alitoka kufunga zaidi ya mabao 30 katika michuano yote katika misimu mitano kati ya sita ya mwisho.
LONDON, ENGLAND: KIGOGO wa zamani wa Arsenal, Keith Edelman amefichua sababu iliyoifanya klabu hiyo kumpiga bei supastaa wao Thierry Henry kwenda Barcelona mwaka 2007.
Henry alikuwa nahodha wa Arsenal wakati huo na alitoka kufunga zaidi ya mabao 30 katika michuano yote katika misimu mitano kati ya sita ya mwisho.
Alisumbuliwa na majeraha msimu mmoja kabla, lakini bado alikwenda kuwa na kiwango bora kabisa kwa miaka mitatu kwenye kikosi cha Barcelona, ambako alifunga mabao 49 katika mechi 121 na kuisaidia miamba hiyo ya Hispania kubeba La Liga mara mbili na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja.
Arsenal ilipokea ada ya Pauni 16 milioni kwenye mauzo ya Henry, lakini Edelman alisema Arsenal ilidhani kilikuwa kipindi mwafaka kumuuza mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwa sababu tayari nyakati zilikuwa zinaanza kumtupa mkono.
Edelman alisema: "Sababu ya kumuuza Thierry kwa sababu alianza kupunguza kasi yake. Soka lake lilikuwa kwenye kasi zaidi. Hivyo, unapopoteza kasi yako, umekwisha. Hivyo, tulipata pesa licha ya kwamba alikuwa akishuka kiwango.
"Kama ilivyo kwa Kevin De Bruyne. Ingekuwa vyema kama angeuzwa ipatikane pesa mwaka jana. Kubaki naye ni tatizo."
Baada ya Henry kuondoka, Arsenal ilishindwa kubeba taji lolote kubwa hadi iliponyakua Kombe la FA mwaka 2014 na hadi sasa timu hiyo bado inataabika haijaziba pengo lake.
Henry alikuwamo kwenye kikosi cha Arsenal isiyoshindika, wakati iliponyakua ubingwa wao wa mwisho wa Ligi Kuu England msimu wa 2003-04 bila ya kupoteza mechi hata moja katika 38 za msimu, ambapo kwenye kikosi chao kulikuwa na mastaa wengine matata kama Patrick Vieira, Robert Pires, Sol Campbell, Gilberto Silva na Kolo Toure.