Isak bado ni pasua kichwa
Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Sweden ameweka wazi dhamira yake ya kutaka kuhama kabla ya dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi halijafungwa Jumatatu ijayo, ambapo moyo wake umeshachagua kujiunga Liverpool, ambayo ofa yao ya kwanza iligomewa na hawaonekani kama wanaweza kufikia kiwango kinachohitajika na Newcastle cha Pauni 150 milioni.
NEWCASTLE, ENGLAND: STRAIKA, Alexander Isak ameripotiwa kushikilia mpango wake wa kutaka kuachana na maisha ya St James’s Park licha ya kuzungumza na mabosi wakubwa wa Newcastle United.
Staa huyo wa kimataifa wa Sweden ameweka wazi dhamira yake ya kutaka kuhama kabla ya dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi halijafungwa Jumatatu ijayo, ambapo moyo wake umeshachagua kujiunga Liverpool, ambayo ofa yao ya kwanza iligomewa na hawaonekani kama wanaweza kufikia kiwango kinachohitajika na Newcastle cha Pauni 150 milioni.
Mwenyekiti wa Newcastle, Yasir Al-Rumayyan anajaribu kuzuia kila kitu kuhakikisha Isak anaendelea kubaki St James’s Park.
Wakurugenzi wa klabu hiyo, Jamie Reuben na Jacobo Solis walikwenda kufanya mazungumzo na Isak nyumbani kwake Jumatatu iliyopita kabla ya Newcastle kukipiga na Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu England.
Mazungumzo hayo yalilenga kumshawishi Isak ili aendelee kubaki Newcastle, arudi kuungana na wenzake mazoezini baada ya kukosa mechi mbili za kwanza za kikosi hicho kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Lakini, Isak ameweka wazi kwamba hajabadili mawazo yake kwamba anataka kwenda kujiunga na Liverpool. Isak alitoa taarifa kwa umma wiki iliyopita akiwashutumu mabosi wa klabu hiyo kuvunja ahadi walizowekeana na kusema uhusiano wake na klabu hiyo hauwezi kuendelea.
Licha ya jitihada kubwa za Newcastle kutaka kumtuliza Isak aendelee kuwapo kwenye kikosi chao, hali ilivyo sakata hilo linaweza kuendelea hadi dirisha la usajili litakapofungwa. Kwa sasa haionekani kama Newcastle itamuuza ili ipate mrithi wa kuja kuvaa buti zake kutokana na muda uliobaki kabla ya dirisha la usajili kwenye majira haya ya kiangazi huko Ulaya kufungwa.