Huu Mtihani mkubwa kwa Liverpool

Muktasari:
- Jumamosi, tovuti ya Daily Mail iliripoti kuwa Real Madrid bado wana imani ya kumsajili Trent Alexander-Arnold katika dirisha la uhamisho lijalo la majira ya joto na vyanzo kutoka Hispania vikadai dili hilo liko karibu kukamilika.
LIVERPOOL, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa Manchester United, Gary Neville amewatahadharisha mabosi wa Liverpool kuwa wanakutana na gharama za kulipa Pauni 250 milioni kwa ajili ya kuboresha kikosi chao ikiwa wataruhusu wachezaji wao watatu waondoke mwisho wa msimu huu.
Jumamosi, tovuti ya Daily Mail iliripoti kuwa Real Madrid bado wana imani ya kumsajili Trent Alexander-Arnold katika dirisha la uhamisho lijalo la majira ya joto na vyanzo kutoka Hispania vikadai dili hilo liko karibu kukamilika.
Mbali ya Trent, mastaa wengine wanaohusishwa kuondoka ni pamoja na Virgil van Dijk na Mohamed Salah ambao wanawindwa na timu za ndani na nje ya England.
Hadi sasa hakuna mwangaza kutoka kwa Liverpool kuhusu uwezekano wa kuwaongeza mikataba na wanaonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kuondoka zaidi ya kubakia.
Neville anaamini kuondoka kwa wachezaji hao watatu kutawagharimu kiasi hicho cha pesa katika kutafuta mbadala wa kuziba mapengo yao.
Akizungumza kupitia kipindi cha Stick to Football, Neville, alisema: “Msimu ukimalizika na wachezaji hawa watatu wakaondoka, Liverpool itakuwa imeachwa na shimo kubwa la kufukia. Itakuwa ngumu kupata mbadala wao na pengine watatakiwa kutumia robo ya Pauni 1 bilioni kwa ajili ya kufanikisha hilo.
“Unazungumzia mmoja wa washambuliaji bora barani Ulaya, mmoja wa mabeki wa kati bora barani Ulaya na mmoja wa mabeki wa kulia bora barani Ulaya. Ingawa Liverpool wamekuwa bora katika kusajili lakini shimo ambalo litaachwa na hawa watatu litawachapa sana kutokana na gharama.”
Neville pia aliwachana wamiliki wa Liverpool, FSG, kwa jinsi walivyoshughulikia mchakato wa kuwasainisha mikataba mipya mastaa hao.
“Liverpool ndio klabu pekee inayoruhusu mkataba wa mchezaji kumalizika bila kuonyesha dalili za kumsainisha upya lakini bado wanapata matokeo mazuri. Wachezaji watatu bora duniani wana mikataba inayokwisha, lakini Liverpool wameendelea na mambo yao na wanaona sawa, mimi siwezi kukubaliana na hili.”
“Kwa Trent kuondoka, hii siyo jambo la wamiliki kusamehewa. Iwe unapitia machafuko kwenye bodi au la, ikiwa wewe ni mmiliki wa klabu na unamtazama Trent miaka miwili iliyopita, hata kama kuna shida lazima uweke mapngo mkakati wa kumsainisha mkataba mpya.”
Kuondoka kwa Alexander-Arnold kutakuwa pigo kubwa kwa Liverpool kwani si tu amekulia katika akademi yao, bali pia anachukuliwa kama mmoja wa mabeki bora duniani.
Baada ya kujiunga na akademi yao akiwa na umri wa miaka sita, beki huyo alicheza katika kikosi cha wakubwa kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 18 katika mechi ya EFL Cup dhidi ya Tottenham mwaka 2018.
Habari kuwa Alexander-Arnold yuko karibu kuhamia Madrid ilisababisha mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na shabiki mmoja kupitia mtandao wa X alionekana akichoma moto jezi ya mchezaji huyu.