HII KITU HAIKUBALIKI… Nahodha Arsenal, kocha wawaambia mastaa

Muktasari:
- Arsenal ilipoteza uongozi wake kwenye mechi hiyo baada ya kuongoza 1-0 kabla ya kuchapwa 2-1, kikiwa kipigo kilichowatokea siku chache kabla ya kukabiliana na Paris Saint-Germain kwenye mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
LONDON, ENGLAND: NAHODHA wa Arsenal, Martin Odegaard amewaambia wachezaji wenzake kwenye kikosi hicho kwamba kipigo cha mabao 2-1 walichokumbana nacho dhidi ya Bournemouth, jana Jumamosi "haikubaliki".
Arsenal ilipoteza uongozi wake kwenye mechi hiyo baada ya kuongoza 1-0 kabla ya kuchapwa 2-1, kikiwa kipigo kilichowatokea siku chache kabla ya kukabiliana na Paris Saint-Germain kwenye mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Timu hiyo ya kocha Mikel Arteta si tu itakwenda kukabiliana na PSG kwenye mechi hiyo Jumatano, bali inatambua kwamba ipo nyuma kwa bao 1-0 ililofungwa katika mechi ya kwanza, huku kwenye Ligi Kuu England baada ya hapo itakabiliana na Liverpool na Newcastle United. Na hilo ndilo lililomfanya nahodha wa timu hiyo, kiungo Odegaard kutoa maneno makali baada ya mechi.
Odegaard, ambaye aliasisti bao la Declan Rice, alisema: "Ni huzuni kubwa. Nadhani tulianza vizuri, tulipata bao na tulionekana tumetawala mchezo kwenye kila kitu, lakini walipofunga, tukapoteza umiliki wa mchezo.
"Tulishindwa kurudi kwenye ubora wetu baada ya pale, kilikuwa kiwango cha hovyo sana kutoka kwetu. Kile kipindi cha pili hakikubaliki kabisa. Yatupasa kusonga mbele kuna mechi muhimu mbele yetu. Tujiweke tayari na kuuchambua huu mchezo vizuri.
"Hicho ndicho tunachotaka, tunataka kuwa washindani kwenye michuano yote. Tulitaka kuja hapa kucheza vizuri na kushinda mechi, lakini hilo halikutokea. Tuna mechi muhimu Jumatano, lakini yatupasa kutumia hii mechi kama maandalizi ya kuifunga PSG Jumatano."
Kocha, Arteta aliunga mkono kauli ya kiungo huyo na alisema: "Tulipata nafasi nyingi sana za kufunga, hatukufanya hivyo. Unaporuhusu mabao kwa mipira ya kutenga ni ngumu kupata pointi tatu."
Aliongeza: "Tulipoteza pointi hapa pia dhidi ya Crystal Palace, Fulham na Brentford - ni kitu tunachohitaji kukiboresha. Tulikuwa na nafasi nyingi, tulitengeneza nafasi kubwa za kufunga, hatukufunga."