He! Yamal amponza mrembo Hispania

Muktasari:
- Fati, 30, aliripotiwa kutumia wikiendi moja na staa huyo wa Barcelona, Yamal, 17 na kuibua uvumi kwamba huenda wawili hao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi.
BARCELONA, HISPANIA: MREMBO mwenye ushawishi mkubwa mitandaoni, Fati Vazquez amefichua kutumiwa meseji za vitisho baada ya kuibuka uvumi kuwa kwenye uhusiano na kinda wa Barcelona, Lamine Yamal kufuatia picha walizotuma kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha mazingira yanayofanana.
Fati, 30, aliripotiwa kutumia wikiendi moja na staa huyo wa Barcelona, Yamal, 17 na kuibua uvumi kwamba huenda wawili hao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Picha walizoshea kwenye kurasa zao za Instagram zilizotofautiana kwa siku tatu, zilionyesha walikuwa mapumziko kwenye mazingira yanayofanana kwa maana ya eneo moja.
Yamal, 17, aliposti picha kwenye mtandao wa kijamii inayomwonyesha akiwa kwenye boti na nyuma yake kukiwa na mwamba mkubwa. Mrembo, Fati naye aliposti picha Instagram inayoonyesha eneo kama hilo.
Yamal aliposti picha inayomwonyesha amejilaza mbele ya bwawa la kuogelea na mbele yake kuna mti, sawa na picha aliyoposti Fati na kuwafanya watu kuamini wawili hao walikuwa pamoja.
Fati mwenye asili ya Galicia, Kaskazini mwa Hispania ana karibu wafuasi 400,000 kwenye ukurasa wake wa Instagram na zaidi ya wafuasi 320,000 huko TikTok.
Mashabiki baada ya kuona picha hizo walianza kuamini wawili hao ni wapenzi, hadi hapo mtu mwingine mwenye ushawishi mkubwa mtandaoni, Javi De Hoyos, aliposema si wapenzi kwa sababu amezungumza na Yamal mwenyewe.
Kwa mujibu wa Hoyos ni kwamba Yamal hakuwa peke yake kwenye mtoko huo, alikuwa na wachezaji wenzake na watu wengine wa Barcelona, hivyo inawezekana Fati alikuwapo kwa ajili ya mtu mwingine na si kinda huyo wa La Masia. Mrembo, Fati - ambaye ni mhitimu wa elimu ya uhudumu wa ndege, alisema amepokea meseji za vitisho na kuombewa kifo tangu alipoposti picha.