He! Sikia hii ya Viktor Gyokeres
Muktasari:
- Ndugu wa wakala aliyehusika kwenye dili la Gyokeres anaripotiwa kujikuta katikati ya sakata hilo lililotokea Stockholm, Sweden.
STOCKHOLM, SWEDEN: POLISI nchini Sweden imeripotiwa kufanya uchunguzi tukio la kufyatuliwa kwa risasi iliyodaiwa ulikuwa mpango wa kumteka mtu aliyehusika kwenye uhamisho wa straika mpya wa Arsenal, Viktor Gyokeres, aliyenaswa kwa Pauni 64 milioni dirisha hili akitokea Sporting Lisbon.
Ndugu wa wakala aliyehusika kwenye dili la Gyokeres anaripotiwa kujikuta katikati ya sakata hilo lililotokea Stockholm, Sweden.
Rais wa Sporting Lisbon, Frederico Varandas, timu ya zamani ya Gyokeres, alisema asingeweza kulazimishwa na kitu chochote katika kukubali uhamisho wa mchezaji huyo kwenda Arsenal.
Polisi wa Sweden wanakabiliwa na uongozeko la uhalifu na sasa imeanzisha uchunguzi kama tukio la kufyatuliana risasi lilihusiana na suala la usajili. Inachunguzwa kama tukio hilo lililotokea Huddinge karibu na mji wa Stockholm kulikoripotiwa jaribio la mauaji dhidi ya mwanafamilia mmoja wa wakala ambaye alihusika kwenye usajili wa straika huyo.
Kulikuwa na uvumi ndugu huyo wa wakala alipata mgawo kwenye ada ya Pauni 64 milioni na hicho ndicho kilichodaiwa kusababisha tukio hilo.
Polisi ilikimbilia haraka kwenye eneo hilo baada ya raia kuripoti. Hata hivyo, hakukuwapo na yeyote aliyejeruhiwa.
Wakala wa Gyokeres hakuthibitisha wala kukataa kuwapo kwa tukio hilo la ndugu yake kutekwa ili akatoe pesa, lakini alisema: “Hii ni tasnia yenye matatizo mengi, hivyo vitu kama hivyo bahati mbaya vinaweza vikitokea.”
Baadaye alisema: “Ufyatuaji huo wa risasi haukumusu yeye wala soka.”
Mkuu wa kitengo maalumu cha polisi huko Sweden, Per Engström, alisema wahalifu wamekuwa wakiwalenga mawakala wa soka kwa miaka ya karibuni kwa sababu wamekuwa wakipokea pesa nyingi.