Haya hapa majanga ya Mbappe

Muktasari:
- Kwa kuanzia, mwaka jana alishindwa kujiunga na PSG katika maandalizi ya msimu akikosekana katika baadhi ya mechi za mwanzo wa Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1) kutokana na mgogoro alioingia na mabosi wa timu hiyo baada ya kuwagomea kusaini mkataba mpya.
PARIS, UFARANSA: KILA inayoitwa leo, maisha ya Kylian Mbappe katika soka yamekuwa yanazidi kuandamwa na sintofahamu kutokana na matukio mbalimbali yanayomtokea.
Kwa kuanzia, mwaka jana alishindwa kujiunga na PSG katika maandalizi ya msimu akikosekana katika baadhi ya mechi za mwanzo wa Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1) kutokana na mgogoro alioingia na mabosi wa timu hiyo baada ya kuwagomea kusaini mkataba mpya.
Mbappe alikuwa akitaka kujiunga na Real Madrid na hilo amelifanikisha msimu huu, lakini huko nako mambo si shwari upande wake. Inaelezwa amekuwa na ugomvi na baadhi ya mastaa wenzake ambao wanaamini amekwenda kuwachukulia nafasi zao. Uwepo wa Mbappe umeripotiwa kuleta mpasuko katika vyumba vya kubadilishia nguo vya Madrid. Mbappe hakufunga katika mechi tatu za kwanza akiwa na Real Madrid, huku wiki kadhaa zilizopita pia akihusishwa kuwa alifanya unyanyasaji wa kijinsia katika hoteli moja nchini Sweden, ambako vyombo vya habari vya nchi hiyo havikutaja jina lake, lakini hoteli aliyofikia ndipo lilifanyika hilo tukio.
Wanasheria wake walitafutwa na vyombo vya habari vya Ufaransa kuzungumzia hilo, lakini walikanusha wakisema ni taarifa za uongo zenye lengo la kumchafua Mbappe. Katika michuano ya Euro mwaka huu pia alifunga bao moja tu kwenye mechi sita alizocheza.
Ukiondoa hayo yote, hivi sasa staa huyo ameachwa kabisa katika timu ya taifa ya Ufaransa itakayoingia kambini kucheza mechi za Uefa Nations League dhidi ya Israel na Italia, licha ya kuzungumza na kocha Didier Deschamps kwamba yupo tayari kuichezea Ufaransa. Awali, katika kalenda ya Fifa iliyopita staa huyo alimwambia Deschamps kwamba anataka kupumzika na kujiweka sawa kabla ya kurejea, hivyo asimuite licha ya kwamba hakuwa majeruhi. Inaelezwa ombi hilo licha ya kukubaliwa na benchi la ufundi, lakini halikumpendeza hata kidogo Deschamps ambaye ameamua kumuacha kuelekea mechi zijazo.
Akitangaza uteuzi wa nyota wake, Deschamps alikiri: “Nilikuwa na mazungumzo mara kadhaa na Mbappe na nikachukua uamuzi wa kumuacha kwa sasa. Ninaweza kusema kwamba ni kweli Kylian alitaka kujumuishwa katika timu, lakini nilimuacha sio kwa sababu za nje ya uwanja, nimefanya uchaguzi wa wachezaji hawa kwa sababu ya kile ninachokitaka. Nafikiri kutokuwepo kwake ni bora.”
Kwa mujibu wa tovuti ya L’Equipe, Mbappé na Deschamps walizungumza kwa siku tatu kabla ya kocha huyo kutangaza kikosi na ilielezwa nyota huyo alikuwa akiamini kwamba atajumuishwa kwenye kikosi.
Inadaiwa kuwa siku ya mwisho Deschamps alimwambia kwamba atamwacha kwa ajili ya kumlinda na tovuti ya RMC, imeripoti kuwa Mbappe alimshukuru kocha huyo kwa kumjulisha mapema.
Hata hivyo, taarifa nyingine zimefichua kwamba mazungumzo baina ya wawili hao hayakuwa mazuri na hilo lilionekana katika kauli za Deschamps alipokuwa anajibu kuhusu kumuacha nyota huyo.
“Hatuwezi kukubaliana kila wakati, lakini ni mazungumzo ninayopaswa kuwa nayo kwa wachezaji. Sipo hapa kwa ajili ya wachezaji kuniambia mimi ni mzuri na bora kuliko wote. Ninasikiliza na huwa najifunza kila wakati kutokana na mazungumzo na wachezaji wangu. Ninapaswa nizungumze nao kabla ili kuweka mambo sawa. Naamini nimefanya uamuzi bora.”