Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hawajawahi kupoteza mechi ya Ligi Kuu ambayo walifunga bao

Muktasari:

  • Lakini, kuna wachezaji hao suala la kuzipa bahati timu zao ili zishinde tu na zipoteze limekuwa la kawaida kwao, wanachohitaji wakali hao ni kufunga tu. Hakika kuna wanasoka 10 wanaoshikilia rekodi tamu kabisa ya kichawi, kwamba wao wanapofunga kwenye mechi za Ligi Kuu England, basi timu zao haziwezi kupoteza mechi hizo.

ASIKWAMBIE mtu Ligi Kuu England ni ngumu kweli kweli. Kushinda au kutoka sare ni jambo linalohitaji nguvu kubwa kuweza kulipata.

Lakini, kuna wachezaji hao suala la kuzipa bahati timu zao ili zishinde tu na zipoteze limekuwa la kawaida kwao, wanachohitaji wakali hao ni kufunga tu. Hakika kuna wanasoka 10 wanaoshikilia rekodi tamu kabisa ya kichawi, kwamba wao wanapofunga kwenye mechi za Ligi Kuu England, basi timu zao haziwezi kupoteza mechi hizo.

10. Victor Moses

Amefunga mechi 19 (ushindi 13, sare 6)

Victor Moses kwa sasa yupo kwenye kikosi cha Chelsea, lakini ndani ya Ligi Kuu England staa huyo wa Nigeria amepita pia kwenye timu za Wigan Athletic, Liverpool, Stoke City na West Ham United. Moses alikuwa chaguo la kocha Antonio Conte, lakini mambo yamekuwa tofauti tangu Maurizio Sarri alipotua Stamford Bridge kuchukua mikoba ya kuinoa timu hiyo.

Lakini, kitu ambacho Sarri hakifahamu ni kuhuzu zali alilokuwa nalo mchezaji huyo kwamba anapofunga kwenye mechi ya Ligi Kuu England tu, basi ujue siku hiyo, Chelsea haipotezi mechi. Kwenye ligi, Moses amefunga mabao katika mechi 19 na kati ya mechi hizo, 13 Chelsea ilishinda na sita zilimalizika kwa sare. Hakika ni mchezaji wa aina yake, Chelsea wamekuwa na zali naye kwa kuwa katika kikosi chao.

9. Oscar

Amefunga mechi 19 (ushindi 16, sare 3)

Kiungo wa Kibrazili, Oscar rekodi zake kwenye Ligi Kuu England aliitumikia Chelsea pekee. Baada ya hapo, aliondoka kwenda zake China, ambapo analipwa mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki. Akiwa na Chelsea alionyesha kwamba yeye ni mchezaji muhimu akifunga mabao 38 kwa ujumla wake katika michuano yote. Mwaka 2014 aliamua kuchukua jezi namba 8 iliyokuwa ikivaliwa na gwiji Frank Lampard. Kwenye mechi za Ligi Kuu England, Oscar alifunga katika mechi 19 na mechi hizo, timu yake ya Chelsea iliibuka kwenye ushindi wa mechi 16 na mechi tatu zilimalizika kwa sare. Kwa lugha nyepesi, Oscar hajawahi kupoteza mechi ya Ligi Kuu England ambayo yeye alifunga bao.

8. Lee Sharpe

Amefunga mechi 19 (ushindi 17, sare 2)

Lee Sharpe rekodi zake kwa mechi za Ligi Kuu England alicheza kwenye vikosi vya Manchester United na Leeds United. Staa huyo alifunga mabao 22 katika mechi 145 alizoitumikia Man United, huku mabao yake 17 kwenye idadi hiyo akiyafunga kwenye Ligi Kuu England. Kwenye kikosi cha Leeds alifunga mabao matano ya ligi. Kwa ujumla wake, mabao yake hayo yote 23 ya ligi aliyofunga Lee Sharpe yalikuwa kwenye mechi 19, ambapo mechi 17 kati ya hizo, timu yake iliibuka na ushindi na mechi mbili tu zilizomalizika kwa sare. Lee Sharpe hajawahi kupoteza mechi ya Ligi Kuu England ambayo yeye alifunga bao.

7. Pedro

Amefunga mechi 19 (ushindi 18, sare 1)

Mhispaniola, Pedro aliyewahi kutamba sana kwenye kikosi cha Barcelona, katika Ligi Kuu England yeye anaitumikia Chelsea yenye maskani yake huko Stamford Bridge. Suala la kufunga halijawahi kuwa shida kwa mshambuliaji huyo na hata msimu huu amefunga pia.

Lakini, kitu kinachovutia ni kwamba Pedro ni kama ana hirizi vile, akifunga bao tu, basi ujue kwenye hiyo mechi Chelsea hawapotezi. Staa huyo amefanya hivyo kwenye mechi 19 na kikosi chake cha Chelsea kimeibuka na ushindi kwenye mechi 18 na kutoka sare mechi moja.

6. Antonio Valencia

Amefunga mechi 23 (ushindi 22, sare 1)

Kwenye Ligi Kuu England, Valencia amecheza kwenye vikosi vya Wigan Athletic na sasa anakipiga Manchester United. Hakika, Valencia ni mchezaji ambaye Man United wanatamani sana afunge, kwani kwa mechi ambazo alifanya hivyo kabla ya mechi ya jana kwenye ligi, timu yake imeshinda na kutoka sare moja tu. Valencia alifunga kwenye mechi 23 za Ligi Kuu na mechi 22 timu yake ilishinda na moja tu ilimalizika kwa sare. Beki huyo wa kulia, hajawahi kufunga mabao mawili kwenye mechi moja ya ligi, ambapo kwenye idadi hiyo ya mabao yake, sita alifunga akiwa na Wigan na 17 alifanya hivyo akiwa na jezi za Man United.

5. Oyvind Leonhardsen

Amefunga mechi 28 (ushindi 21, sare 7)

Kwenye Ligi Kuu England, Oyvind alipita kwenye vikosi vya Wimbledon, Liverpool, Tottenham na Aston Villa. Hakika kwenye timu ambazo alipita, mchezaji huyo alifanya vizuri sana lilipokuja suala la mechi za Ligi Kuu England. Mabao yake 13 alifunga akiwa Wimbledon na kwa ujumla wake, Leonhardsen alifunga mabao 30 kwenye ligi hiyo. Kiungo huyo wa Norway, hakika ameacha rekodi katika kila mechi ya Ligi Kuu England aliyofunga, basi timu yake haijapoteza mechi hiyo, ilishinda au kutoka sare na si kupoteza. Baada ya kustaafu mwaka 2007, kwa sasa Leonhardsen anafanya kazi ya kuwa ofisa usafirishaji wa watembeleaji wa huko Arctic.

4. Salomon Kalou

Amefunga mechi 32

(ushindi 29, sare 3)

Chelsea waliwahi kuwa na huduma matata kabisa kutoka kwa Muivory Coast, Salomon Kalou kwenye kikosi chao. Sawa, The Blues walikuwa na mchezaji mwingine pia wa Ivory Coast, ambaye alikuwa matata pia, Didier Drogba, lakini tofauti ya wawili hao ipo sehemu moja tu, Kalou kila alipofunga, basi Chelsea ilijihesabia ushindi kwenye mechi hiyo au sare, hawajawahi kupoteza. Staa huyo alidumu Stamford Bridge kwa miaka sita na kufunga mabao 36 kwenye ligi, huku msimu wake mzuri zaidi kwenye ligi hiyo ulikuwa 2010/11, The Blues ilipokuwa chini ya Carlo Ancelotti.

3. Dele Alli

Amefunga mechi 33

(ushindi 27, sare 6)

Kwenye Ligi Kuu England, Dele Alli ameitumikia Tottenham Hotspur tu. Hajahama na wala huko alikotoka hadi anafika kwenye kikosi cha Spurs, timu yake haikuwa kwenye ligi hiyo. Bado ni kijana mdogo, ambaye ana nafasi kubwa ya kwenda kufanikiwa mbele ya safari. Bao lake la mwisho la Alli lenye mafanikio lilikuwa kwenye ushindi wa Spurs wa mabao 2-1 dhidi ya Newcastle United katika ufunguzi wa Ligi Kuu England. Kwa msimu uliopita alifunga mabao 18, lakini kitu kinachovutia kuhusu Mwingereza huyo ni kwamba kila alipofunga bao kwenye mechi ya ligi, Spurs haijapoteza mechi, inashinda au sare tu.

2. Darius Vassell

Amefunga mechi 46 (ushindi 36, sare 10)

Mshambuliaji Vassell kwenye Ligi Kuu England alipita kwenye timu za Aston Villa na Manchester City. Kwa ujumla wake, Vassell alifunga mabao 52 kwenye Ligi Kuu England, 35 akiwa na kikosi cha Aston Villa na 17 alipokuwa kwenye kikosi cha Man City. Lakini, katika mechi zote za Ligi Kuu England ambazo fowadi huyo alifunga, timu yake haijawahi kupoteza mchezo. Alidumu kwenye ligi hiyo kwa miaka 11 kabla ya kwenda Uturuki na kisha kuja kustaafia Leicester City kipindi hicho ikiwa kwenye Championship.

1. James Milner

Amefunga mechi 47 (ushindi 37, sare 10)

Kwenye Ligi Kuu England, kiraka Milner amecheza kwenye timu za Leeds United, Newcastle United, Aston Villa, Manchester City na sasa Liverpool. Mwingereza huyo ana rekodi ya kipekee, kwenye mechi za Ligi Kuu England ambazo alifunga bao, basi timu yake haijapoteza, inashika au kutoka sare. Alifunga mabao katika mechi tano Leeds, sita Newcastle, 12 akiwa na Aston Villa, 13 na kikosi cha Man City na 12 katika kikosi cha Liverpool yenye maskani Anfield. Kwa ujumla wake, Milner amefunga mabao 49 katika ligi hiyo.