Hawa wanaweza kusepa muda wowote

Muktasari:
- Hawa ni wachezaji watano wanaotikisa soko la usajili ambao wanaweza kukamilisha uhamisho wa kujiunga na timu zinazowataka muda wowote kabla ya dirisha kufungwa.
LONDON, ENGLAND: ZIMEBAKI siku saba kabla ya dirisha la usajili la majira ya kiangazi kufungwa katika zile ligi kubwa Ulaya, ambapo hadi sasa kuna majina ya mastaa wanaoonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuondoka, lakini bado dili hazijakamilika.
Hawa ni wachezaji watano wanaotikisa soko la usajili ambao wanaweza kukamilisha uhamisho wa kujiunga na timu zinazowataka muda wowote kabla ya dirisha kufungwa.
VICTOR OSIMHEN
Nyota huyu anadaiwa kuwa huenda akawa mmoja kati ya washambuliaji ghali watakaosajiliwa na Chelsea siku za mwisho za dirisha la usajili.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameomba kuondoka Napoli katika dirisha hili na hajajumuishwa hata katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kinachoendelea na Ligi Kuu Italia (Serie A).
Sababu ya msingi kwa mshambuliaji huyo kutokamilisha usajili kujiunga na timu yoyote hadi sasa ni Pauni 100 milioni zinazotakiwa na Napoli ili kumuachia.
PSG ni mojawapo wa timu zinazoonekana kwamba zitafanya jambo kwake, kwani inatafuta mbadala wa Kylian Mbappe aliyetua Real Madrid, lakini hadi sasa hakuna muafaka uliofikiwa.
Chelsea inabaki kuwa timu pekee katika vita ya kumtaka kwa sababu Napoli inataka kumchukua Romelu Lukaku baada ya kuondoka kwa Osimhen, hivyo kuna uwezekano timu hizo mbili zikafanya biashara.
IVAN TONEY
Suala la mshambuliaji huyu raia wa England kuondoka Brentford katika dirisha hili linapewa zaidi ya asilimia 90 kutokea.
Hata hivyo, timu nyingi za Ligi Kuu England zinaonekana kusita kutoa pesa ili kumsajili jambo lililosababisha hivi karibuni baadhi ya timu kutoka Saudi Arabia kuingilia kati.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, wawakilishi wa staa huyo kwa sasa wapo Saudia kufanya mazungumzo na Al Ahli kwa ajili ya kuipata saini yake katika dirisha hili.
Timu zinazooonekana kuwa huenda zikafanya kitu England ni pamoja na Manchester United na Arsenal ambazo bado zinatafuta washambuliaji kwa ajili ya kuboresha maeneo ya ushambuliaji.
FEDERICO CHIESA
Federico Chiesa ni miongoni mwa wachezaji wa Juventus ambao waliambiwa watafute timu za kujiunga nazo katika dirisha hili kwa kuwa hawapo katika mipango ya kocha Thiago Motta.
Baada ya taarifa hiyo, taarifa ziliibuka kwamba Liverpool ni miongoni mwa timu zilizo katika mazungumzo na wawakilishi wake ikiwa ni madirisha kadhaa tangu ishindwe kumsajili baada ya kutakiwa kutoa Pauni 82 milioni.
Mbali ya Majogoo hao, Chiesa pia anawindwa na Tottenham Hotspur, Aston Villa, Manchester United na Chelsea ambazo zote zinaonekana kuwa na uwezo wa kutoa Pauni 20 milioni zinazohitajika na Juventus ili kumuachia.
Chiesa ambaye mkataba wake unamalizika mwakani moja kati ya vitu ambavyo timu nyingi zimezirudisha nyuma katika kumsajli ni mshahara wake wa Pauni 180,000 kwa wiki anaoutaka.
MIKEL MERINO
Uhamisho wa Mikel Merino kutua Arsenal bado una uwezekano wa kukamilika licha ya kuchelewa.
Moja kati ya mambo yanayokwamisha uhamisho wa staa huyo ni ada ya uhamisho, kwani inaripotiwa kwamba mchezaji huyo ameshafanya makubaliano binafsi na timu.
Mabosi wa Real Sociedad wanataka kiasi kisichopungua Pauni 30 milioni ili kumuuza na Arsenal wanaona dau hilo ni kubwa kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye mkataba wake unamalizika mwakani.
Ili kumsajili, Arsenal itatakiwa kuuza baadhi ya wachezaji ikiwemo Eddie Nketiah na Aaron Ramsdale ambao wote wanahitajika na timu mbalimbali Ulaya.
EBERECHI EZE
Hadi kufikia sasa Liverpool, Manchester City na Tottenham Hotspur zote zinahitaji huduma yake katika dirisha hili la usajili.
Kwa upande wa Manchester City, mshambuliaji Oscar Bobb atakuwa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa baada ya kuvunjika mguu akiwa mazoezini na Julian Alvarez ameondoka kwenda Atletico Madrid kwa Pauni 82 milioni.
Licha ya uwepo wa Savinho, bado matajiri hao wanahitaji huduma ya mshambuliaji mwingine atakayekwenda kusaidiana na Erling Haaland pale mbele. Katika mkataba wake Eze kuna kipengele kinachomwezesha kuondoka ikiwa timu inayomtaka italipa kiasi cha Pauni 60 milioni ingawa baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa kifungu hicho kilimalizika mapema mwezi huu, hivyo timu inayomtaka itatakiwa kujadiliana na Palace juu ya bei.