Hamilton kukosa mkwanja Mercedes

KITENDO cha dereva bingwa mara saba wa mbio za magari ya langalanga duniani (Formula one), Lewis Hamilton kutokea kampuni ya magari hiyo, Mercedes kukosa taji la ubingwa huo mwaka jana, kilimkosesha bonasi ya Dola 15 milioni.

Bonasi hiyo aliyoikosa msimu uliopita inaenda pia kukosekana kwenye mkwanja aliotakiwa aupate Hamilton baada ya msimu huu unaoendelea, kwani hakuna dalili za wazi za kushinda mbio za mwaka huu ambazo zimetawaliwa zaidi na madereva wa kampuni pinzani, Red Bull, Max Verstappen.

Hii ndio sababu kubwa inayotajwa Hamilton atapishana na bonasi hizo  jumla ya Dola 30 milioni kama alivyosaini mkataba wa kuzipata mwaka 2021, huku mkataba wake ukikaribia mwisho msimu huu.

Hamilton analipwa Dola 27.5 milioni kwa mwaka akiwa nafasi ya pili nyuma ya Verstappen anayelipwa zaidi ya Dola 50 milioni kwa kila msimu. Kama Hamilton angeendelea kushinda mbio mbili mfululizo zilizopita, angebaki juu zaidi ya Verstappen.