Man Utd ikidoda... McTominay, Lukaku wabeba ubingwa Italia

Muktasari:
- Mastaa hao McTominay na Lukaku kila mmoja alifunga bao wakati Napoli ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cagliari, Ijumaa iliyopita wakati kikosi hicho kinachonolewa na kocha Antonio Conte kiliipiku Inter Milan kwa pointi moja kwenye mbio za ubingwa huo wa Scudetto.
NAPLES, ITALIA: NDO hivyo. Mastaa walioonwa si kitu Manchester United, Scott McTominay na Romelu Lukaku wamenyakua taji la Serie A ndani ya wiki moja hiyo hiyo ambayo klabu yao ya zamani ilikumbwa na aibu ya kuchapwa kwenye fainali ya Europa League na kumaliza msimu kichovu.
Mastaa hao McTominay na Lukaku kila mmoja alifunga bao wakati Napoli ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cagliari, Ijumaa iliyopita wakati kikosi hicho kinachonolewa na kocha Antonio Conte kiliipiku Inter Milan kwa pointi moja kwenye mbio za ubingwa huo wa Scudetto.
McTominay, ambaye amekuwa shujaa huko Naples tangu alipojiunga na Napoli akitokea Man United kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, alifunga bao la kwanza kwa staili ya kibaiskeli akiunganisha krosi ya Matteo Politano muda mfupi kabla ya mapumziko katika kipute kilichofanyika uwanjani Stadio Diego Armando Maradona na kuwapagawisha mashabiki.
Bao hilo lilikuwa la 13 kwa McTominay katika msimu wake wa kwanza bora kabisa kwenye soka la Italia, ambapo mkali huyo wa kimataifa wa Scotland alifunga mabao sita katika mechi saba za mwisho kusaidia timu yake kunyakua taji hilo la ubingwa wa Italia.
Napoli ambayo pia kwenye kikosi chake kuna mchezaji mwenzake McTominay wanayecheza pamoja timu ya taifa ya Scotland, Billy Gilmour anayetamba kwenye kiungo, iliongeza bao na ubao kusomeka 2-0 mapema kwenye kipindi cha pili, lililofungwa na Lukaku baada ya pasi ya Amir Rrahmani ambapo straika huyo Mbelgiji aliwakimbiza mabeki wa Cagliari akiwamo Yerry Mina na kufunga bao lake la 14 la msimu.
Ushindi huo umeifanya Napoli kunyakua taji la pili la Serie A katika kipindi cha misimu mitatu, wakati huo nyuma ilikuwa imebeba mara mbili tu - 1986-87 na 1989-90, ilipokuwa na mkali Maradona kwenye kikosi.
Inter yenyewe ilikuwa kibaruani dhidi ya Como inayonolewa na Cesc Fabregas, katika mechi iliyomshuhudia kipa wa zamani wa Liverpool, Pepe Reina, 42, akitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu muda mfupi kabla ya mapumziko, katika mechi yake ya mwisho ya kimashindano.
Como tayari ilikuwa nyuma kwa bao moja wakati kipa anatolewa, beki Stefan de Vrij alipofunga kwa kichwa na kisha Joaquin Correa aliongeza bao la pili mwanzoni kwa kipindi cha pili, kama muda ambao Lukaku aliongezea bao la pili Napoli.
Kikosi hicho cha kocha Conte kilifahamu wazi ushindi ndicho kitu pekee kitakachowapa ubingwa bila ya kujali matokeo ya wapinzani wao, Inter. Kama Napoli ingepoteza kwa Cagliari kisha Inter ikaichapa Como basi mechi ya mchujo ya kupata bingwa ingepigwa wiki ijayo.
Lakini, Napoli haikutaka shida zote hizo na kuamua kushinda, shukrani kwa mabao ya McTominay na Lukaku, ambapo siku mbili zilizopita timu yao ya zamani Man United ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur kwenye fainali ya Europa League na hivyo kumaliza msimu mikono mitupu, huku ikiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ambapo Jumapili itacheza mechi yake ya mwisho dhidi ya Aston Villa uwanjani Old Trafford kuhitimiza msimu wao wa majanga.
McTominay aliibukia kwenye akademia ya Man United na kucheza mechi 255 kabla ya kuuzwa kwa Pauni 25.7 milioni kwenda Napoli, wakati Lukaku alisajiliwa na miamba hiyo ya Old Trafford akitokea Everton mwaka 2017 kwa ada ya Pauni 75 milioni na nyongeza ya Pauni 15 milioni, ambapo alicheza timu hiyo mechi 96 na kufunga mabao 42 kjabla ya kutimkia Inter Milan mwaka 2019.