Haaland bado anaumwa, Arsenal kicheko
Muktasari:
- Haaland alitolewa nje baada ya dakika 45 za kwanza katika mechi dhidi ya Fulham baada ya kupata jeraha dogo, na kwa sasa inaelezwa bado hayupo sawa hali inayoweza kuwa ni faida kwa Arsenal katika mbio zao za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amekiri kuwa Erling Haaland hayuko fiti kwa asilimia 100 baada ya kutoonekana uwanjani katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Salford.
Haaland alitolewa nje baada ya dakika 45 za kwanza katika mechi dhidi ya Fulham baada ya kupata jeraha dogo, na kwa sasa inaelezwa bado hayupo sawa hali inayoweza kuwa ni faida kwa Arsenal katika mbio zao za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Haaland alikuwa amefunga mabao katika mechi mbili zilizotangulia za Man City, ikiwamo bao muhimu ugenini dhidi ya Liverpool wiki iliyopita, lakini hakurejea uwanjani baada ya mapumziko katika ushindi wa hivi karibuni dhidi ya Fulham.
Baada ya mechi dhidi ya Fulham, Guardiola amesema walifanya uamuzi huo kama sehemu ya tahadhari baada ya mshambuliaji huyo kulalamika kuwa ana maumivu katika kipindi cha kwanza.
Akizungumza kabla ya ushindi wa Man City wa Jumamosi kwenye Kombe la FA, Guardiola alikiri kuwa hali ya Haaland bado sio nzuri.
"Erling hayuko fiti kwa asilimia 100," Guardiola aliwaambia waandishi wa habari.
"Sio tatizo kubwa kwa mujibu daktari aliniambia. Lakini alikuwa anapata tabu kabla na wakati mechi inaendelea na ndiyo maana hakucheza kipindi cha pili. Tutaangalia maendeleo yake.”
Ingawa Guardiola alijaribu kupunguza uzito wa tatizo hilo, picha za mazoezi zilizochapishwa na Man Ijumaa hazikumuonyesha Haaland ikiwa ni ishara kwamba hata mazoezi hafanyi.
Man City itakutana na Newcastle kwenye Ligi Kuu wikiendi ijayo mechi ambayo ina umuhimu sana kwenye mbio za ubingwa.
Haaland bado ni nguzo muhimu katika kikosi cha Man City na mabao yake mara nyingi yamekuwa yakisaidia kufufua matumaini ya vita ya ubingwa.