Gyokeres kamwaga mboga Manchester United

Muktasari:
- Straika huyo amepania kufanya uhamisho kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huku Arsenal ikiwa moja ya klabu inayotajwa kuisaka kwa nguvu zote saini ya mkali huyo wa kimataifa wa Sweden.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Straika, Viktor Gyokeres amegomea uhamisho wa kwenda kujiunga na Manchester United, imeripotiwa.
Straika huyo amepania kufanya uhamisho kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huku Arsenal ikiwa moja ya klabu inayotajwa kuisaka kwa nguvu zote saini ya mkali huyo wa kimataifa wa Sweden.
Man United ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kumchukua Gyokeres kutokana na kocha wake Ruben Amorim kufahamiana vyema na mshambuliaji baada ya kumnoa walipokuwa pamoja Sporting CP.
Lakini, kwa mujibu wa gazeti moja la Ureno la Record, mshambuliaji ameamua kuachana na mpango wa kwenda Old Trafford na badala yake Arsenal ndiko mahali anakoweza kuibukia kwa sasa.
Mabosi wa Man United wameripotiwa kuwa kwenye mawasiliano na mabosi wenzao wa Sporting pamoja na mchezaji Gyokeres, lakini walishindwa kumshawishi mshambuliaji huyo ili kuchagua kwenda Old Trafford, ambako mashetani wekundu hawatashiriki katika michuano yoyote ya Ulaya baada ya kuwa na msimu mbovu na kumaliza katika nafasi 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu wa 2024-25.
Kuhusu Arsenal, nayo iliripotiwa kwamba ofa yao ya Pauni 55 milioni kwa ajili ya mchezaji huyo ilikataliwa na Sporting.
Jambo hilo ndilo linalodaiwa kumkasirisha Gyokeres, ambaye aliripotiwa kwamba awali alifikia makubaliano na klabu yake hiyo kwamba kama kuna timu itakayotoa dau hilo, basi ikubali ili aondoke.
Arsenal ipo kwenye mchakato wa kuandaa ofa ya pili kwa ajili ya Gyokeres, lakini sasa ni suala la wakala wa mchezaji huyo na mabosi wa Sporting kukubaliana na kipengele kinachotaja bei anayouzwa kilichowekwa kwenye mkataba. Kinachoelezwa ni kwamba Sporting inataka ilipwe Pauni 84 milioni kama ilivyobainishwa kwenye mkataba.
Rais wa Sporting, Frederico Varandas alisema kwamba hawezi kushawishika kabisa na kumwachia mshambuliaji huyo aondoka kwa pesa ndogo kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Alisema: “Sporting haitakubali kabisa kudanganyika vyovyote vile, nadhani watanifahamu vyema sasa.”
Jambo hilo limedaiwa kumweka kwenye mgogoro mkubwa baina ya mchezaji na klabu.
Straika Gyokeres alijibu wakati alipoulizwa kama anapendezwa na maisha ya London baada ya kuhusishwa na uhamisho wa kwanza Arsenal, alisema: “Maneno yamekuwa mengi kwa sasa, mengi ni ya uongo. Nitazungumza muda sahihi utakapofika.”
Taarifa hizo za kukataliwa na Gyokeres ni pigo kubwa kwa Man United, ambayo kwenye dirisha hili hili imeshakataliwa na straika Liam Delap, aliyetimkia zake Chelsea.
Na sasa Man United inamtazama Victor Osimhen kama chaguo mbadala, lakini shida inakuja kwenye mshahara anaotaka alipwe Mnigeria huyo, Pauni 500,000 kwa wiki, huku staa wa zamani wa Old Trafford, Rio Ferdinand, akiwaambia waajiri wake wa zamani straika wa kumsajili ni Osimhen na si Gyokeres ambaye anaona Ligi ya England itamsumbua.