Liverpool yamgeukia Anthony Gordon

Muktasari:
- Inaelezwa mazungumzo baina ya Liverpool na Newcastle juu ya staa huyo yalifanyika dirisha lililopita la majira ya kiangazi na sasa yanaendelea yalipoishia.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL inaangalia uwezekano wa kufanya dili la Pauni 100 milioni la kumsajili nyota wa Newcastle, Anthony Gordon.
Inaelezwa mazungumzo baina ya Liverpool na Newcastle juu ya staa huyo yalifanyika dirisha lililopita la majira ya kiangazi na sasa yanaendelea yalipoishia.
Inalezwa, Newcastle ilitaka kumuuza Gordon mwaka jana kwa sababu ilikuwa katika hali mbaya ya kifedha na ilihitaji mapato ili kuepuka rungu la kukiuka sheria za matumizi ya pesa.
Hata hivyo, kwa sasa hali yao ya kiuchumi sio mbaya, lakini huenda ikalazimika kumuuza tena baada ya Liverpool kutua na ofa nono.
Gordon, ambaye ni shabiki wa Liverpool tangu utotoni, alihamia St James Park kutoka Everton kwa Pauni 45 milioni, Januari 2024.
Alisaini mkataba mpya Oktoba mwaka jana na msimu uliopita alifunga mabao sita na kutoa pasi tano za mabao kwenye EPL.
Liverpool imepanga kufanya matumizi makubwa dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuimarisha kikosi cha Arne Slot kilichoshinda taji msimu uliopita.
Hadi sasa tayari wamemsajili beki wa kulia wa kimataifa wa Uholanzi, Jeremie Frimpong kutoka Bayer Leverkusen kwa Pauni 29.5 milioni.
Vilevile ipo katika hatua za mwisho kukamilisha dili la kumsajili mchezaji mwingine kutoka timu hyo, kiungo Florian Wirtz anayetajwa atasajiliwa kwa Pauni 116 milioni, pia inatarajia kuipata huduma ya beki wa kushoto wa Bournemouth, Milos Kerkez anayeuzwa kwa Pauni 40 milioni.
Mbali ya mastaa hao, mapema mwezi huu tovuti ya The Sun ilifichua Liverpool ilikuwa na nia ya kumsajili Bradley Barcola wa PSG.
Inaelezwa moja kati ya sababu zinazoifanya Liverpool imgeukie Gordon ni kutokuwa na uhakika wa kuendelea kusalia na Luis Diaz ambaye amewekewa ofa nono na waarabu wa Saudi Arabia, pia anawindwa na Barcelona.
Vilevile straika raia wa Uruguay, Darwin Nunez naye anawindwa na Atletico Madrid na timu za Saudi Arabia.
Kabla ya Gordon, Liverpool pia walionesha nia ya kumsajili Alexander Isak lakini walirudi nyuma haraka baada ya kutajiwa inahitajika Pauni 150 milioni.