Gundogan chochote kinaweza kutokea

Muktasari:
- Miamba ya soka ya Uturuki, Galatasaray inapambana kunasa saini ya Gundogan, 34, ambaye amebakiza mwaka mmoja tu kwenye mkataba wake huko Etihad.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amemfungulia milango ya kutokea kiungo Ilkay Gundogan dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kukiri wachezaji wengi watauzwa.
Miamba ya soka ya Uturuki, Galatasaray inapambana kunasa saini ya Gundogan, 34, ambaye amebakiza mwaka mmoja tu kwenye mkataba wake huko Etihad.
Kocha Guardiola, ambaye alimrudisha Gundogan kwenye kikosi chake mwaka jana, alisema anamtegemea Mjerumani huyo kwenye mipango ya klabu yake kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani.
Lakini, Guardiola alikiri kikosi chake cha sasa ni kikubwa sana, hivyo kuna wachezaji ni lazima wafunguliwe mlango wa kutokea ili kubaki na wachache ambao watapata nafasi ya kucheza na kusaidia timu.
Alipoulizwa kuhusu hatima ya Gundogan, Guardiola alisema: “Sina habari, habari njema. Hivyo, sifahamu chochote, sijazungumza naye na kama hatakuwa kwenye mipango, basi hatakuwapo. Lakini, kwa sasa yupo naye kwenye timu. Hatuwezi kwenda msimu ujao na wachezaji 26 au 27 kwa sababu hawatakuwa na muda wa kucheza, hivyo kuna wachezaji wachache wataondoka.
“Kwa wakati huu, Ilkay yupo kwenye mipango yangu na timu. Ningependa kubaki na wachezaji waliopo kwa sasa kwa msimu wote. Ningependa iwe hivyo. Sijawahi kuwa na malalamiko yoyote juu ya tabia za wachezaji.”
Man City inajiandaa pia kuwafungulia mlango mastaa wawili wa England, Kyle Walker na Jack Grealish, wakati Rodri ikiwa bado hatima yake haijafahamika vyema wakati huu akiwa anajaribu kujiweka sawa baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kwa msimu uliopita kutokana na kusumbuliwa na jeraha la goti.