Guardiola asababisha hofu kubwa Man City
Muktasari:
- Man City, ambao wanakanusha vikali tuhuma hizo, wamekuwa katika vita vya kisheria na viongozi wa ligi kwa zaidi ya miaka mitatu sasa wakikabiliwa na mashtaka hayo 115 yanayohusisha pia udanganyifu katika matumizi ya pesa kwenye usajili.
MANCHESTER, ENGLAND: RIPOTI zinafichua watu wa ndani wa Manchester City wameanza kupata hofu juu ya uwezekano wa Pep Guardiola kuondoka kwenye kikosi hicho kuliko hata hukumu ya mashtaka 115 yanayowakabili kwenye Ligi Kuu England.
Man City, ambao wanakanusha vikali tuhuma hizo, wamekuwa katika vita vya kisheria na viongozi wa ligi kwa zaidi ya miaka mitatu sasa wakikabiliwa na mashtaka hayo 115 yanayohusisha pia udanganyifu katika matumizi ya pesa kwenye usajili.
Usikilizwaji wa kesi hiyo ulimalizika Desemba 2024, lakini hadi sasa bado hakuna uamuzi uliotolewa. Iwapo Man City itapatikana na hatia, wanaweza kukumbana na adhabu mbalimbali zikiwemo faini kubwa au kupokonywa pointi.
Hata hivyo, kwa waliopo ndani huko Etihad, mustakabali usio na uhakika wa Guardiola unasababisha wasiwasi mkubwa zaidi. Gazeti la The Telegraph linaripoti kuwa chumba cha kubadilishia nguo cha Man City kinafahamu vyema mipango mbadala inayopangwa endapo kocha huyo ataondoka mwishoni mwa msimu.
Mkataba wa Guardiola unaendelea hadi majira ya joto ya 2027, lakini mara kwa mara amedokeza kuwa atazungumzia mustakabali wake mwaka huu. Kocha huyo kutoka Catalan atatimiza miaka kumi tangu achukue mikoba ya kuinoa Man City huku ndani ya muda huo ameshinda kila taji lililowezekana, yakiwemo mataji sita ya Ligi Kuu England.
Hata hivyo, mwaka huu wa kalenda umeanza vibaya kwa Man City, ikishindwa kupata ushindi katika mechi za ligi na kupokea kipigo cha aibu dhidi ya Bodoe/Glimt kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki.
Akizungumza baada ya kipigo cha 3-1 kutoka Bodoe/Glimt, Guardiola alikiri kuwa “kila kitu kilikuwa kinaenda vibaya.” Kwa mujibu wa ripoti, mwenendo wa Guardiola katika uwanja wa mazoezi haujabadilika licha ya sintofahamu kuhusu mustakabali wake, na anaonekana kujituma kama kawaida katika kujaribu kuirejesha Man City kileleni.