Pep Guardiola awasifu Arsenal, kisha achimba mkwara
Muktasari:
- Hata hivyo, kocha wa The Gunners, Mikel Arteta anasisitiza kuwa kikosi chake bado kiko mbali na ukamilifu, na kwamba Man City ya Guardiola haiwezi kuondolewa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
MANCHESTER, ENGLAND: PEP Guardiola amewamwagia sifa vinara wa Ligi Kuu England, Arsenal, akiwataja kama timu bora zaidi duniani kwa sasa.
Hata hivyo, kocha wa The Gunners, Mikel Arteta anasisitiza kuwa kikosi chake bado kiko mbali na ukamilifu, na kwamba Man City ya Guardiola haiwezi kuondolewa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Man City ilikuwa nyuma kwa pointi saba dhidi ya Arsenal kabla ya mechi ya Jumamosi dhidi ya Wolves na hilo limekuja baada ya chama hilo la Guardiola kushindwa kupata ushindi kwenye mechi zao nne za mwisho kwenye ligi.
Guardiola alisema: “Wao (Arsenal) ni timu bora zaidi duniani kwa sasa. Tunapaswa kuboresha kiwango chetu na kutumaini watatupa nafasi moja ya kuwafikia.”
Man City ya Pep ina historia ya kuwafukuzia na kuwavuka Arsenal, baada ya kuwazidi katika misimu ya 2022–23 na 2023–24.
Manchester United wataitembelea Emirates, leo Jumapili kwa mchezo wa ligi, huku Arsenal ikitoka kwenye mechi nne za ugenini mfululizo katika mashindano tofauti ikiwa bado wanapambana katika Ligi ya Mabingwa, Kombe la FA na Kombe la Ligi.
Kocha Arteta alisema: “Huhitaji kurudi mbali kwenye historia ya klabu hiyo (Man City) katika miaka kumi iliyopita na kile wanachoweza kufanya. Tunajua tunachopaswa kufanya ili kushinda Ligi Kuu. Bado tuko mbali na kuwa wakamilifu.”
Guardiola alikosa wachezaji 11 wakati Man City iliposhtushwa kwa kipigo cha 3–1 kutoka kwa Bodoe/Glimt katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumanne iliyopita.
Nyota wapya waliosajiliwa dirisha hili, Marc Guehi na Antoine Semenyo walitarajia kuwapo uwanjani Wolves, huku Bernardo Silva akirejea baada ya adhabu ya kusimamishwa. Na kwenye hilo, Guardiola aliongeza: “Najua sababu ya sisi kuwa kwenye matatizo kwa sasa kwa asilimia 100 najua kinachoendelea na timu.
“Wachezaji wamechoka, kama ilivyokuwa msimu uliopita, hatuwezi kuzungusha kikosi. Kwa sasa, hatuwezi kucheza dhidi ya timu za Ulaya kila baada ya siku tatu. Kwa hiyo, hebu tupe muda kidogo zaidi. Je, itatosha? Sijui.
“Tutakapofika Februari au Machi, ninachokiomba nipate kikosi changu kamili. Baada ya hapo, naapa, tutakuwa pale. Nirudishieni wachezaji wangu kisha tutaona kitakachotokea. Nina timu ya kipekee na sina shaka yoyote kuhusu hilo.”