Pep Guardiola azua hofu Manchester City
Muktasari:
- Man City imekuwa ikikanusha vikali mashtaka hayo 115 yanayohusu ukiukwaji wa kanuni za masuala ya kifedha na kesi imekuwa ikiunguruma kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.
MANCHESTER, ENGLAND: VIONGOZI wa Manchester City wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kocha wa timu hiyo, Pep Guardiola kuondoka mapema kuliko hata hukumu ya mashtaka 115 inayotarajiwa kutajwa hivi karibuni.
Man City imekuwa ikikanusha vikali mashtaka hayo 115 yanayohusu ukiukwaji wa kanuni za masuala ya kifedha na kesi imekuwa ikiunguruma kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.
Kesi hiyo ilihitimishwa Desemba 2024, lakini hadi sasa hukumu bado haijatolewa na ikiwa Man City itapatikana na hatia, inaweza kukumbana na adhabu mbalimbali ikiwemo faini kubwa na hata kupokonywa pointi.
Hata hivyo, kwa mabosi wa juu hatma isiyoeleweka ya Guardiola ndio inayowatia hofu kubwa zaidi. Gazeti la The Telegraph linaripoti, vigogo hao kwa sasa wanaumiza kichwa ni kocha gani anayeweza kuchukua mikoba ya Mhispania huyo aliyeripotiwa anaweza kung'atuka tangu wiki iliyopita.
Mkataba wa Guardiola unatarajiwa kumalizika majira ya kiangazi mwaka 2027, lakini amekuwa akidokeza mara kwa mara atazungumzia mustakabali wake mwaka huu.
Kocha huyo mzaliwa wa Catalonia atatimiza miaka 10 akiwa na Man City kwa msimu huu, huku akiwa amejizolea mafanikio kibao ikiwemo mataji sita ya Ligi Kuu England.
Hata hivyo, msimu huu umeanza vibaya kwa Man City, ikishindwa kupata matokeo mazuri katika mechi za ligi na kupokea kipigo cha aibu kutoka Bodo/Glimt katika Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki.
Akizungumza baada ya kipigo cha mabao 3-1 katika Uwanja wa Arctic Circle, Guardiola alikiri; “Kila kitu kilikuwa kikienda vibaya kwa upande wake na timu.”
Kwa mujibu wa ripoti, mwenendo wa Guardiola katika uwanja wa mazoezi haujabadilika licha ya sintofahamu kuhusu mustakabali wake na anaonekana kujitoa kikamilifu na kuonyesha juhudi za kuirejesha Man City kileleni.
Tetesi kuhusu hatma yake ziliongezeka mwanzoni mwa wiki hii, baada ya mtangazaji wa zamani wa Sky Sports, Richard Keys kudai kocha huyo yuko mbioni kuondoka.
“Nadhani ni wazi kabisa ataondoka mwishoni mwa msimu,” amesema Keys katika beIN Sport baada ya Man City kupokea kipigo dhidi ya Man United Old Trafford.
“Lakini anaweza akaondoka hata wiki hii na najua akiondoka basi Enzo Maresca atachukua usukani. Man City watakasirika sana na bila shaka watakanusha haya ninayo yasema, lakini hilo limo akilini mwake, nakuambia."
Hata hivyo, utabiri wa Keys haukukamilika na Guardiola alionekana uwanjani katika mechi dhidi ya Wolves na Man City iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kuzidi kuizamisha Wolves chini ya msimamo ikiburuza mkia kwa pointi nane ilizopata baada ya mechi 23.