Guardiola afuta bonasi Man City

Muktasari:
- Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England watakwenda Marekani kwenye fainali za Kombe la Dunia na Kocha Guardiola alisema kwa kiwango cha mastaa wake wa msimu huu, hata kama watakwenda kushinda taji hilo, hakuna bonasi wanastahili kupewa, hata zawadi ya saa hawatakiwi kupewa.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema mastaa wa kikosi hicho hawastahili kabisa kupewa bonasi msimu huu hata kama watakwenda kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia la Klabu.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England watakwenda Marekani kwenye fainali za Kombe la Dunia na Kocha Guardiola alisema kwa kiwango cha mastaa wake wa msimu huu, hata kama watakwenda kushinda taji hilo, hakuna bonasi wanastahili kupewa, hata zawadi ya saa hawatakiwi kupewa.
Man City imeonekana kuwekeza nguvu kwenye kufanya vizuri katika michuano hiyo ya Fifa itakayofanyika majira yajayo ya kiangazi kwa kuwa yana zawadi kubwa ya pesa. Mshindi ataweka kibindoni Pauni 100 milioni, pesa ambayo hutolewa kwa timu inayoshika nafasi ya chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa msimu mzima kutokana na malipo ya haki ya matangazo ya televisheni na zawadi nyingine ya pesa.
Man City imekuwa ikiwapa bonasi wachezaji na wafanyakazi wake, lakini kocha Guardiola alisema hakuna yeyote kwenye timu hiyo anayestahili bonasi kutokana na kiwango chao kibovu wanachokionyesha uwanjani msimu huu.
Guardiola alisema: “Hatustahili hicho kitu msimu huu. Hatustahili bonasi ya msimu huu. Bonasi, kama unashinda, sijui ni kiasi gani. Tunakwenda kushinda ni ishu ya klabu, makocha na wafanyakazi na wachezaji, hatustahili bonasi, hata saa hatustahili.”
Mastaa wa Man City walipokea karibu Pauni 2 milioni kila moja wakati iliposhinda mataji matatu kwa msimu mmoja misimu miwili iliyopita, nusu ya hiyo ilitokana na mafanikio yao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Guardiola anatarajia kukiongoza kikosi chake kwenye mchezo wa Kombe la FA na itakipiga na Bournemouth, kwenye mchezo wa robo fainali wa kombe hilo utakaofanyika Jumapili.
Guardiola anafukuzia rekodi ya kuwamo kwenye orodha ya makocha wanne tangu ilipofanyika Vita ya Dunia ya Pili kushinda ubingwa wa Kombe la FA kwa mara ya tatu. Makocha wengine waliofanya hivyo ni Bill Nicholson, Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger.