Gabriel Jesus amvuruga Arteta

Muktasari:
- Mbrazili huyo alianzishwa katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Man United jana Jumapili, lakkini hakumaliza, dakika 40 alipata maumivu ya goti yaliyoonekana kuwa siriazi, wakati alipoonekana kuwa na maumivu makali na nafasi yake akaingizwa Raheem Sterling.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta ameonyesha wasiwasi juu ya afya ya straika Gabriel Jesus aliyeumia na kuhitaji msaada wa machela kutolewa kwenye mechi dhidi ya Manchester United.
Mbrazili huyo alianzishwa katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Man United jana Jumapili, lakkini hakumaliza, dakika 40 alipata maumivu ya goti yaliyoonekana kuwa siriazi, wakati alipoonekana kuwa na maumivu makali na nafasi yake akaingizwa Raheem Sterling.
Na kocha Arteta hakutoa maneno mazuri juu ya majeraha hayo ya Jesus aliposema: “Wasiwasi mkubwa hicho ndicho ninachohisi. Alilazimika kutoka uwanjani kwa machela. Hilo unaweza kuona hali ilivyo kuwa ngumu.”
Kukosekana kwa Jesus kumeongeza idadi ya majeruhi kwenye kikosi hicho cha Arsenal, ambapo wagonjwa wengine kwenye kikosi hicho ni Ben White, Takehiro Tomiyasu, Bukayo Saka na Ethan Nwaneri.
Majeraha hayo yanaifanya Arsenal kuwa kwenye ulazima wa kufanya usajili kwenye dirisha hili la Januari. Lakini, kabla ya mechi hiyo ya Man United hilo wala halikuwa kwenye mpango wa Arteta.
Alipoulizwa kabla ya mechi hiyo kama Arsenal inahitaji mshambuliaji mpya dirisha la mwezi huu, alijibu: “Hapana, mambo yanabadilika kutokana na majeruhi tuliopata wengi na ni wachezaji wakubwa, sawa inawezekana, kwa sababu kama huyo mchezaji tunayemtaka atakuja kutufanya kuwa bora.”