Everton wamalizana na kiungo Hayden
Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na Middlesbrough, na sasa anaondoka katika klabu ambayo alijiunga nayo tangu akiwa kwenye kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 10, baada ya kushindwa kupanda Ligi Kuu ya England msimu uliopita.
LONDON, England: EVERTON imemsajili kiungo Hayden Hackney kutoka Middlesbrough kwa ada ya angalau pauni16 milioni.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na Middlesbrough, na sasa anaondoka katika klabu ambayo alijiunga nayo tangu akiwa kwenye kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 10, baada ya kushindwa kupanda Ligi Kuu ya England msimu uliopita.
Hackney, ambaye alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Championship msimu wa 2025/26, aliisaidia Middlesbrough kufika fainali ya mchujo wa kupanda daraja mwezi Mei, lakini walifungwa mabao 1-0 na Hull City.
"Ninafuraha kuwa hapa," alisema Hackney, ambaye amesaini mkataba wa miaka mitano na Everton.
"Mara tu nilipozungumza na kocha (David Moyes), na nilipofahamu kuwa Everton walikuwa wananitaka, kwa kweli nilijua kwamba ningechagua Everton."
"Ni klabu kubwa, ina uwanja mpya na inaelekea kwenye mwelekeo mzuri. Nilitamani kuwa sehemu ya safari hiyo."
Hackney ameichezea Middlesbrough mechi 154 na kufunga mabao 16.
Katika taarifa yake, Middlesbrough ilisema: "Wakati kiungo huyu aliyekulia katika akademi ya klabu akianza sura mpya ya maisha yake ya soka, kila mmoja ndani ya MFC anamtakia Hayden kila la heri katika maisha yake ya baadaye."
Wakati huohuo, Everton pia ipo karibu kukamilisha makubaliano na Chelsea ya kumsajili winga Tyrique George, baada ya mchezaji huyo kucheza kwa mkopo katika klabu hiyo kipindi cha pili cha msimu uliopita.