Ancelotti: Sir Ferguson pekee anaweza kunikosoa
Muktasari:
- Kocha huyo wa Brazil, mwenye umri wa miaka 67, amekuwa akikosolewa katika kampeni hii ya Kombe la Dunia.
DALLAS, Marekani: KOCHA Carlo Ancelotti amesema atakubali kukosolewa na mtu mmoja pekee anayemwona kuwa ana sifa za kufanya hivyo ni Sir Alex Ferguson.
Kocha huyo wa Brazil, mwenye umri wa miaka 67, amekuwa akikosolewa katika kampeni hii ya Kombe la Dunia.
Mabingwa hao mara tano wa dunia walianza mashindano kwa sare ya 1-1 dhidi ya Morocco, kabla ya kuzifunga Haiti na Scotland na kumaliza kileleni mwa Kundi C kwa ubora wa tofauti ya mabao.
Katika hatua ya 32 bora, Brazil ilipata ushindi wa taabu dhidi ya Japan baada ya kutoka nyuma na kushinda kwa bao la dakika ya 96 lililofungwa na Gabriel Martinelli.
Hata hivyo, mashabiki wengi wa Brazil bado hawajaridhishwa na kiwango cha timu chini ya Ancelotti, licha ya kuwa na rekodi ya mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 31 ya ukocha wake. Katika kipindi hicho, ameshinda mataji ya ligi katika nchi zote tano kubwa za Ulaya pamoja na mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumza kabla ya mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Norway, ambapo mshindi atatinga robo fainali, Ancelotti alijibu wakosoaji wake kwa kusema:"Nchini Italia kuna msemo unaosema kwamba kila mwanaume anataka kuwa kocha na kila mwanamke anataka kuwa mbunifu wa majengo. Sijui kama ninaielewa soka au la, lakini hakuna anayepaswa kunihukumu kuhusu hilo."
"Jambo moja la uhakika ni kwamba nimeongoza kwa zaidi ya mechi 1,400. Huenda hiyo haitoshi kuthibitisha kuwa ninaelewa soka, lakini ni uzoefu mkubwa sana.
Aliongeza kusema "kuna mtu mmoja tu ambaye ameongoza mechi nyingi zaidi yangu naye ni Alex Ferguson, ambaye ameongoza kwa zaidi ya mechi 2,000."
Ancelotti aliendelea kusema:
"Ninapokea ushauri kutoka kwa kila mtu, lakini mtu pekee ambaye anaweza kweli kuwa sahihi kunipa ushauri ni Alex Ferguson.
"Nina uhakika kwa asilimia 100 kwamba mimi si geniasi, lakini wakati huohuo nina uhakika kwa asilimia 100 kwamba mimi si mjinga."
Hata hivyo, nguli wa soka wa Norway Kjetil Rekdal anaamini kuwa presha yote ipo kwa Ancelotti na Brazil kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya Norway inayoongozwa na Erling Haaland.
Cha kushangaza, Brazil haijawahi kuifunga Norway katika mechi zao nne zilizopita. Isitoshe, ilipoteza dhidi yao katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia mwaka 1998.
Katika mchezo huo, Jose Oliveira Bebeto aliwapa Brazil bao la kuongoza mwishoni mwa mchezo, lakini Tore Andre Flo na Kjetil Rekdal waligeuza matokeo katika dakika za mwisho na kuipa Norway ushindi wa kihistoria.
Rekdal, ambaye alifunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti katika mechi hiyo, anatabiri kuwa historia itajirudia tena.
Alisema:"Norway itashinda 2-1. Historia hujirudia katika soka, na hilo hutokea mara nyingi.Brazil ndiyo yenye presha kubwa zaidi.
"Daima kutakuwa na hofu hiyo, hofu ya kwamba watajikwaa tena dhidi ya Norway."