Eriksen kurudi kucheza EPL

LONDON, ENGLAND. KIUNGO Christian Eriksen yupo mbioni kujiunga na moja ya timu kutoka Ligi Kuu England hata hivyo hajafahamika ni wapi ambapo atatua.

Eriksen hajacheza mechi yoyote tangu alipopata shambulio la moyo kwenye mechi ya Kombe la Euro 2020 mwaka jana, Denmark ilipokuwa ikimenyana na Finland.

Kwa sasa Eriksen hana timu ya kuichezea baada ya kuvunja mkataba na Inter Milan ambayo alikuwa akiichezea kabla ya majanga hayo kumkuta.

Taarifa zimeripoti timu kibao za Ligi Kuu England zimeonyesha kumsajili kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa eneo la kati.

Kiungo huyo wa Kimataifa wa Denmark aliwahi kuichezea Tottenham kuanzia msimu wa 2013 hadi 2020 alipotimika na kujiunga na Inter Milan, Eriksen alikuwa tegemeo na amefunga jumla ya mabao 69 katika mechi 305 alizocheza Spurs.

Hivi karibuni Antonio Conte aliwahi kusema mlango upo wazi kiungo huyo kurejea Tottenham.

“Sijazungumza na Eriksen muda kidogo, ni faraja kumuona akicheza tena uwanjani., tunazungumzia kuhusu mchezaji muhimu, ni kijana mzuri kilichomtokea mwaka jana ni hatari sana, hata mimi niligopa sana, nadhani milango ipo wazi siku zote kama ikitokea akataka kurudi nyumbani,” alisema Conte.