Enzo Fernandez akili yote inawaza PSG
Muktasari:
Kiungo huyo wa Argentina alijiunga na The Blues mwaka 2023 kwa ada iliyovunja rekodi wakati huo ya Pauni 106 milioni.
LONDON, ENGLAND: ENZO Fernandez anafikiria kwa makini mustakabali wake Chelsea na huenda akawashangaza wengi kwa kuachana na miamba hiyo.
Kiungo huyo wa Argentina alijiunga na The Blues mwaka 2023 kwa ada iliyovunja rekodi wakati huo ya Pauni 106 milioni.
Hata hivyo, inadaiwa aliachwa na maumivu makubwa baada ya kuondoka kwa Enzo Maresca siku ya Mwaka Mpya 2026.
Sasa, kuna uwezekano kiungo huyo akaandaa safari ya kuondoka Stamford Bridge.
Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, naibu nahodha huyo mwenye umri wa miaka 24 hana mpango wa kulazimisha uhamisho dirisha la Januari.
Badala yake, uhamisho wa majira ya joto unaonekana kuwa na uwezekano mkubwa zaidi. Ripoti hiyo inaongeza kuwa mabingwa wa Ulaya, Paris Saint-Germain wanapanga dili kubwa sana ili kumsajili Fernandez.
Endapo ataamua kuhamia Parc des Princes, atalazimika kushindana na wachezaji kama Vitinha, Joao Neves na Fabian Ruiz kwa nafasi za kucheza katika kiungo. Nyota huyo wa zamani wa Benfica ana mkataba Chelsea hadi 2032.
Aling’ara sana chini ya Maresca, akivaa mara kwa mara kitambaa cha unahodha kutokana na matatizo ya majeraha ya Reece James.
Fernández alishinda Kombe la Conference League na Kombe la Dunia la Klabu la FIFA mwaka jana na tayari ameshinda Kombe la Dunia na Copa América akiwa na timu ya taifa ya Argentina. Hata hivyo, Fernández huenda asiwe usajili unaopendwa na mashabiki wa PSG.
Katika sherehe za Copa América mwaka 2024, alionekana kwenye video akiimba nyimbo za kibaguzi dhidi ya wachezaji Weusi wa Ufaransa, miaka miwili baada ya kuifunga Ufaransa kwenye fainali ya Kombe la Dunia.
Fernández alianza michezo miwili chini ya kocha wa muda Calum McFarlane dhidi ya Manchester City na Fulham ikiwemo kufunga bao la kusawazisha la dakika za mwisho katika Uwanja wa Etihad.
Aliingia kama mchezaji wa akiba katika ushindi wa Kombe la FA dhidi ya Charlton, kisha akacheza dakika zote 90 katika mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Arsenal Jumatano, ambapo Chelsea ilipoteza mabao 3-2, ikiwa chini ya kocha mpya Liam Rosenior.
Fernández ameifungia Chelsea jumla ya mabao 24 katika mechi 145 alizocheza.