Enzo avunja ukimya wa hatma yake ya kutua Madrid
Muktasari:
- Fernandez alizungumza baada ya kuifungia Argentina bao la ushindi katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Misri, uliowapeleka mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia hatua ya robo fainali.
MIAMI, Marekani: KIUNGO wa Chelsea, Enzo Fernandez amekataa kuzungumzia hatma yake katika klabu hiyo huku tetesi za kuhusishwa na Real Madrid zikiendelea kushika kasi katika dirisha hili la usajili.
Fernandez alizungumza baada ya kuifungia Argentina bao la ushindi katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Misri, uliowapeleka mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia hatua ya robo fainali.
Kwa muda sasa, kiungo huyo amekuwa akitajwa kuondoka Stamford Bridge, huku Real Madrid ikitajwa kuwa moja ya klabu zinazomuwania. Hata hivyo, miamba hiyo ya Hispania walitoa taarifa rasmi wakikanusha kuwa na mpango wa kumsajili mchezaji huyo.
Akizungumza na DAZN baada ya mchezo huo, Fernandez alisema kwa sasa anajikita kikamilifu kwenye majukumu ya timu ya taifa.
"Sifikirii kuhusu mustakabali wangu kwa sasa. Niko hapa nikifurahia wakati huu ambao ni wa kipekee kwangu. Baada ya Kombe la Dunia kumalizika, ndipo tutaona kitakachofuata," alisema.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya wakala wake, Javier Pastore, kueleza tena kuwa mteja wake anaweza kuondoka Chelsea, huku akieleza kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwa kujiunga na Real Madrid kungekuwa hatua nzuri kwake.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hadi sasa Chelsea haijapokea mawasiliano yoyote rasmi kutoka Real Madrid kuhusu kuanza mazungumzo ya usajili wa Fernandez, licha ya uvumi unaoendelea kusambaa.
Katika taarifa yake rasmi, Real Madrid ilisisitiza kuwa haijafanya hatua yoyote ya kumfuata kiungo huyo na wala haina mpango wa kufanya hivyo.
Klabu hiyo ilieleza kuwa inamheshimu Fernandez kama mmoja wa viungo bora duniani, pia ina uhusiano mzuri wa kiutawala na Chelsea na haitaki kuhusishwa na taarifa zisizo na ukweli.
"Real Madrid haijafanya mawasiliano yoyote, moja kwa moja au kupitia mtu mwingine, yenye lengo la kumsajili Enzo Fernandez. Aidha, klabu haina nia ya kufanikisha uhamisho huo," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Real Madrid pia ilieleza kusikitishwa na kuendelea kusambazwa kwa taarifa ambazo, kwa mujibu wa klabu hiyo, hazina msingi wa ukweli na zinachanganya mashabiki pamoja na kuathiri taswira ya klabu na wahusika.
Licha ya tamko hilo, taarifa zinaeleza kuwa Real Madrid iliwahi kumweka Fernandez kwenye orodha ya viungo waliokuwa wakifuatiliwa, lakini Chelsea ilisimama kidete kwa kutangaza kuwa haitamuuza kwa chini ya pauni120 milioni.
Vyanzo vya ndani ya Stamford Bridge vinaeleza kuwa viongozi wa Chelsea hawana haraka ya kumuachia nahodha msaidizi huyo na wako tayari kuendelea naye iwapo hakuna klabu itakayofikia kiwango cha fedha wanachokitaka.
Katika dirisha hili la usajili, Real Madrid tayari imefanya biashara na Chelsea baada ya kumsajili beki wa kushoto Marc Cucurella kwa ada ya pauni51.8 milioni.
Akiwa na kikosi cha Hispania kwenye Kombe la Dunia, Cucurella aliwahi kumshawishi hadharani Fernandez kuhamia Santiago Bernabeu, kauli iliyozua mjadala miongoni mwa mashabiki wa Chelsea.
Fernandez pia aliwahi kukiri hadharani kuwa angependa kuishi jijini Madrid siku moja. Kauli hiyo ilimuweka matatani msimu uliopita, ambapo alipewa adhabu ya ndani ya klabu ya kutocheza mechi mbili wakati Chelsea ilikuwa chini ya kocha Liam Rosenior.
Mbali na Real Madrid, klabu za Paris Saint-Germain, Atletico Madrid na Manchester City nazo zimekuwa zikitajwa kufuatilia kwa karibu hali ya kiungo huyo wa kimataifa wa Argentina.