Duh! Kumbe Amorim ndo hivi...
Muktasari:
- Chanzo cha ndani kutoka Old Trafford kimefichua kocha huyo raia wa Ureno alikuwa amevunjika moyo sana baada ya ugomvi mkubwa uliozuka kati yake na mkurugenzi wa michezo, Jason Wilcox, Ijumaa kabla ya Man United kucheza dhidi ya Leeds huko Elland Road, kiasi cha kuwaambia marafiki zake kuwa anaondoka kwenye timu hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: RIPOTI za ndani zinadai kocha wa zamani wa Manchester United, Ruben Amorim alikuwa tayari kujiuzulu siku tatu kabla ya kufukuzwa kazi na alikuwa tayari hata kusamehe fidia ya Pauni 12 milioni ambayo kwa sasa timu hiyo inatakiwa kumlipa.
Chanzo cha ndani kutoka Old Trafford kimefichua kocha huyo raia wa Ureno alikuwa amevunjika moyo sana baada ya ugomvi mkubwa uliozuka kati yake na mkurugenzi wa michezo, Jason Wilcox, Ijumaa kabla ya Man United kucheza dhidi ya Leeds huko Elland Road, kiasi cha kuwaambia marafiki zake kuwa anaondoka kwenye timu hiyo.
Hata hivyo, inaelezwa alibadilisha msimamo huo baada ya kuzungumza na wakala wake, Raul Costa, ambaye alisisitiza klabu inapaswa asubiri kwanza aidha wazungumze na klabu ili mambo yawe sawa au afukuze rasmi ili kupewa stahiki zake kwani kama angejiuzulu wakati huo, inaaminika angeondoka bila kupata hata senti moja ya fidia.
Costa aliona ishara zote Man United ilikuwa ikienda kumfukuza Amorim hivyo, alisisitiza asianze kujiuzulu yeye kwa sababu angepoteza pesa nyingi.
Amorim aliitwa kwenye kikao na Wilcox pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) Omar Berrada Jumatatu na akafukuzwa kazi papo hapo.
Kitendo hicho kilimwezesha Amorim kupata fidia kubwa ya takribani Pauni 12 milioni ambayo ilisababisha kufikia kiasi cha Pauni 100 milioni ambacho Man United imewalipa makocha iliowafukuza tangu kuondoka kwa kocha Sir Alex Ferguson.
Baada ya kuondoka kwake sasa, Man United imemteua Michael Carrick kama kocha wa muda kuchukua nafasi ya Amorim atakayefundisha hadi mwisho wa msimu.
Carrick ameshaanza kazi tangu mwanzoni mwa wiki hii na atakuwa na kibarua cha kwanza kigumu dhidi ya Manchester City kesho Jumamosi.
Kabla ya Carrick, timu ilikuwa chini ya Darren Fletcher aliyesimamia kwa mechi mbili ambazo moja ni dhidi ya Leeds iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2 katika Ligi Kuu England, pia wakapoteza mechi ya FA kwa mabao 2-1 dhidi ya Brighton.