Fomesheni nne za kocha Man United!
Muktasari:
- Gwiji huyo wa Mashetani Wekundu anarejea kwenye benchi la ufundi la Old Trafford kwa mara ya pili baada ya kumshinda Ole Gunnar Solskjaer katika kuwania nafasi hiyo ya kuwa kocha wa muda Man United.
MANCHESTER, ENGLAND: MICHAEL Carrick anaweza kuanzisha mambo mapya Manchester United kwa kukiandaa kikosi kitakachocheza kwenye njia nne tofauti akiwa kocha wa muda.
Gwiji huyo wa Mashetani Wekundu anarejea kwenye benchi la ufundi la Old Trafford kwa mara ya pili baada ya kumshinda Ole Gunnar Solskjaer katika kuwania nafasi hiyo ya kuwa kocha wa muda Man United.
Carrick, ambaye aliwahi kuinoa Man United pia kwa muda wakati Solskjaer alipofukutwa 2021, sasa anatarajiwa kuiongoza miamba hiyo ya Old Trafford, ambapo mechi yake ya kwanza itakuwa ya Manchester derby dhidi ya Manchester City, Jumamosi.
Carrick atakuwa na matumaini ya kufanya vizuri zaidi kuliko Darren Fletcher, ambaye aliongoza timu hiyo kwenye mechi mbili mechi mbili kama kocha wa kipindi cha mpito baada ya Ruben Amorim kuonyeshwa mlango wa kutokea.
Hata hivyo, bado haijulikani Carrick atatumia fomesheni gani katika mechi yake ya kwanza akiwa amerejea Man United. Katika kipindi chake kifupi cha miaka minne iliyopita, Carrick alitumia mifumo kadhaa ya uchezaji katika mechi tatu alizoongoza.
Alitumia mfumo wa 4-3-3 katika ushindi dhidi ya Villarreal na Arsenal.
Pia alitumia mfumo wa 4-3-1-2 katika sare ya 1-1 dhidi ya Chelsea, ambao kwa nyakati fulani uliendana na mpangilio wa Chelsea wa 3-4-2-1.
Mfumo wa kawaida wa mabeki wanne unaonekana kuwa chaguo kubwa zaidi, hasa baada ya Fletcher kuurudisha katika mechi zake mbili, sare dhidi ya Burnley na kipigo cha kwenye Kombe la FA kutoka kwa Brighton.
Mfumo wa 4-3-3, au mbadala wake 4-2-3-1, ungeweza kumwona Bruno Fernandes akicheza nafasi ya Namba 10 nyuma ya Benjamin Šeško kama mshambuliaji wa kati. Amad Diallo na Bryan Mbeumo wamerejea kutoka kwenye majukumu ya Afcon na huenda wakachukua nafasi za Mason Mount na Matheus Cunha kwenye winga.
Wakati huo huo, Casemiro na Kobbie Mainoo huenda wakapewa nafasi kwenye safu ya kiungo cha kati badala ya Manuel Ugarte. Katika safu ya ulinzi ya mabeki wanne, inatarajiwa kuwa Diogo Dalot, Leny Yoro na Lisandro Martínez waanze, huku Matthijs de Ligt akiwa majeruhi na Noussair Mazraoui bado yuko kwenye mashindano ya Afcon 2025 huko Morocco.
Uamuzi pia utahitajika kufanywa katika nafasi ya beki wa kushoto, huku Luke Shaw akiwa tayari kucheza baada ya kupumzishwa dhidi ya Brighton, ambapo Patrick Dorgu alicheza badala yake. Iwapo Carrick ataamua kuwa Amorim alikuwa sahihi na akaendelea na mfumo wa mabeki watatu, tatizo la Shaw na Dorgu kucheza pamoja litatatuliwa, huku Dalot na Diallo wakipigania nafasi ya beki wa kulia wa pembeni (wing-back).
Cunha na Mount pia wanaweza kurejea katika mipango ya Carrick. Lakini kama kocha huyo mpya ataamua kwenda njia isiyotegemewa, anaweza pia kuchagua mfumo wa 4-3-1-2. Mfumo huo mwembamba ungetegemea mabeki wa pembeni kushambulia juu sana.
Hata hivyo, ungeweza kuwatoa kiwango bora wachezaji wengi wa kati ambao Man United wanamiliki katika safu ya ushambuliaji.
Chaguo jingine ni kutumia mfumo wa jadi wa 4-4-2 wenye mtindo wa umbo la almasi katikati ya uwanja, ambao unaweza kuipa timu hiyo uwiano mzuri zaidi na pia kuamsha kumbukumbu za enzi za mafanikio chini ya kocha Sir Alex Ferguson.