Djigui Diarra mtu na nusu, aibeba Mali Afcon 2025
Muktasari:
- Mali imefanikiwa kuibuka na ushindi wa penalyi 3-2 dhidi ya Tunisia baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya kuchezwa kwa dakika 120.
CASABLANCA , MOROCCO: KIPA, Djigui Diarra amekuwa shujaa wa Mali iliyocheza na wachezaji 10 uwanjani baada ya kuokoa penalti mbili kuifanya timu yake kuichapa Tunisia na kutinga robo fainali ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 uliochezwa usiku wa Jumamosi.
Mali imefanikiwa kuibuka na ushindi wa penalyi 3-2 dhidi ya Tunisia baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya kuchezwa kwa dakika 120.
El Bilal Toure alifunga penalti ya ushindi baada ya Ali Abdi mkwaju wake kudakwa na golikipa wa Mali, Diarra, ambaye aliokoa penalti mbili kati ya tano za Tunisia, ambapo moja ilipaa juu ya goli.
Baada ya mechi ambayo haikuwa na amshaamsha nyingi mpaka dakika za mwisho, kipindi cha penalti kilikuwa na drama nyingi kwani nahodha wa Mali, Yves Bissouma alipiga juu na mwenzake Nene Dorgeles kupiga mpira kwenye nguzo.
Mali walikuwa chini kwa mchezaji mmoja kwa zaidi ya saa moja na nusu baada ya Woyo Coulibaly kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumkanyaga Hannibal Mejbri.
Tunisia ilipata bao la kuongoza dakika mbili za mwisho baada ya kichwa cha Firas Chaouat kiliingia kwenye lango la Diarra, lakini Mali ilipewa penalti katika dakika za majeruhi baada ya Yassine Meriah kunawa moira ndani ya boksi.
Lassine Sinayoko alifunga penalti hiyo na kuupeleka mchezo kwenye muda wa ziada wa dakika 30. Chaouat alidhani amefunga bao la pili mapema katika kipindi cha pili cha muda wa ziada lakini bao hilo lilighairishwa kwa kosa la kuotea.
Mali itasafiri kuelekea Tangier kukabiliana na mabingwa wa Afcon 2021 Senegal katika robo fainali siku ya Ijumaa wiki hii.