Senegal yapiga tatu, yatinga robo fainali
Muktasari:
- Mabao mawili ya Pape Gueye, aliyofunga kwenye kipindi cha kwanza yaliifanya Senegal kupindua meza na kuichapa Sudan, ambayo iliangulia kwa bao la Aamir Abdallah.
TANGIER, MOROCCO: SENEGAL imekuwa timu ya kwanza kutinga robo fainali ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya kuichapa Sudan mabao 3-1 katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliofanyika uwanjani Grand Stade de Tangier, usiku wa Jumamosi.
Mabao mawili ya Pape Gueye, aliyofunga kwenye kipindi cha kwanza yaliifanya Senegal kupindua meza na kuichapa Sudan, ambayo iliangulia kwa bao la Aamir Abdallah.
Abdallah alifunga kwa ustadi mkubwa akimchambua kipa mahiri Edouard Mendy kwenye dakika ya sita ya mchezo na hivyo kuwapa furaha ya mapema mashabiki wa Sudan huko Tangier.
Baadaye, kipa Mendy alilazimika kufanya kazi ya ziada kumgomea Mohamed Eisa kufunga bao la pili, kabla ya Senegal kujibu mapigo na kufunga mara mbili na kwenda mapumziko ikiwa 2-1.
Straika Nicolas Jackson alikaribia kufunga, lakini shuti lake alilopiga akiwa karibu kabisa na goli la Sudan liliokolewa na kipa Monged Elneel, sekunde chache kabla ya Gueye kufunga kwa shuti la chinichini akiwa nje ya mita 18.
Kiungo huyo wa Villarreal, Gueye, ambaye muda mwingi alikuwa akitengenezea nafasi nje ya boksi la Sudan, alipata fursa nyingine na kufunga kwa mguu wa kushoto akimteka kipa Elneel.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, huku Sudan ikijaribu kusaka bao la kusawazisha na Mendy alilazimika kufanya kazi ya ziada kumgomea beki wa kulia, Sheddy Barglan, lakini Simba wa Teranga ndiyo walikuwa na siku njema katika mechi hiyo.
Kinda wa Paris Saint-Germain, Ibrahim Mbaye aliyeingia kutokea benchini alikuja kuimaliza mechi hiyo baada ya kufunga bao na hivyo kuifanya Senegal kujihakikishia tiketi yake ya kutinga robo fainali ya mikikimikiki hiyo ya Afcon 2025, ambapo itakipiga na mshindi baina ya Mali na Tunisia, mechi iliyofanyika usiku huo wa Jumamosi. Mechi ya robo fainali itafanyika Ijumaa, Januari 9, 2026.