Dakika 90: Kuvunja urafiki wa Haaland, Bellingham
Muktasari:
- Mbali na ushindani wao uwanjani, Haaland na Bellingham wanajulikana kuwa na urafiki wa karibu ulioanzia walipokuwa wachezaji wa Borussia Dortmund mwaka 2020.
MIAMI, Marekani: WATU wengi wamewahi kucheza soka dhidi ya marafiki zao, lakini si wengi wanaoweza kusema walikutana uwanjani katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia. Hilo ndilo litakalowakuta Erling Haaland na Jude Bellingham watakapokutana Jumamosi katika mchezo wa kusisimua utakaofanyika Miami, Florida.
Mbali na ushindani wao uwanjani, Haaland na Bellingham wanajulikana kuwa na urafiki wa karibu ulioanzia walipokuwa wachezaji wa Borussia Dortmund mwaka 2020.
Wawili hao walitua katika klabu hiyo ya Bundesliga kwa wakati mmoja na haraka wakawa moja ya pacha hatari zaidi, huku mashabiki wakivutiwa na ushirikiano wao ndani ya uwanja.
Urafiki wao uliendelea kukua licha ya baadaye kujiunga na vigogo wawili wanaoshindana barani Ulaya, Manchester City na Real Madrid.
Kutokana na ukaribu wao, mashabiki mitandaoni wamekuwa wakiwalinganisha na wahusika wa tamthilia maarufu Heated Rivalry, inayohusu mapenzi kati ya wachezaji wa mchezo wa ice hockey.
Mitandao ya kijamii pia imejaa video na picha zinazoonyesha namna wawili hao wanavyolindana na kusaidiana. Mojawapo ni tukio ambalo Haaland, mwenye urefu wa futi 6 na inchi 4, alimkingia kifua Bellingham wakati alipokuwa akibishana na mchezaji wa timu pinzani.
Tukio lingine lililozua gumzo ni pale Bellingham alipomkaribia Haaland wakati wa mahojiano na kumpa busu la utani shavuni, jambo lililowapa mashabiki sababu zaidi ya kuzungumzia urafiki wao.
Baada ya England kuiondoa Mexico na Norway kuitoa Brazil, mastaa hao sasa wanatarajiwa kuwa mahasimu kwa dakika 90 katika robo fainali ya Kombe la Dunia.
Licha ya utani mwingi unaoendelea mitandaoni, hakuna kinachoashiria zaidi ya urafiki wa kawaida kati yao. Wengi wanaamini ni moja ya urafiki imara zaidi katika soka la kisasa, huku kila mmoja akiheshimu uwezo wa mwenzake na kufurahia mafanikio yake.
Bellingham alikuwa na umri wa miaka 17 tu alipohamia Borussia Dortmund akitokea Birmingham City na akaandika historia kwa kuwa mfungaji mwenye umri mdogo zaidi wa klabu hiyo katika mechi yake ya kwanza.
Haikuchukua muda mrefu kabla Haaland hajaanza kumsifia kiungo huyo wa England.
"Bellingham ana umri wa miaka mitatu chini yangu. Hilo linashangaza. Ni mchezaji wa ajabu," alisema Haaland mwaka 2021.
Kwa upande wake, Bellingham alisema:
"Kila wiki nasema jinsi alivyo mchezaji bora. Kiwango mnachokiona si bahati. Anafanya kazi kwa bidii kila siku, na kama binadamu ni bora hata kuliko alivyo mshambuliaji."
Haaland alipojiunga na Manchester City mwaka 2022, urafiki wao haukukoma.
Bellingham aliwahi kufichua kuwa mshambuliaji huyo wa Norway alikuwa akimtumia ujumbe wa kumtia moyo wakati England ilipokuwa ikicheza Kombe la Dunia nchini Qatar.
"Siku zote hunitia moyo. Alinitumia ujumbe kabla na baada ya mechi ya kwanza akinitakia kila la heri, kisha akanipongeza. Ni mtu mzuri sana. Tunawasiliana mara kwa mara," alisema Bellingham.
Aliongeza kuwa mazungumzo yao mengi huwa ni ya utani.
"Tunapotokuwa bize na mechi huwa tunatumiana vitu vya kuchekesha au mambo ambayo tumewahi kuyazungumzia."
Baada ya England kutolewa na Ufaransa katika Kombe la Dunia la mwaka 2022, Haaland pia alimfariji rafiki yake kwa kuandika kwenye chapisho lake la Instagram: "Mchezaji wa kiwango cha juu," ujumbe uliopata maelfu ya alama za kupenda.
Kwa sasa, wote wawili wameendelea kung'ara katika klabu zao, huku Haaland akiwa tegemeo la Manchester City na Bellingham akifanya makubwa Real Madrid, wakitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji hatari zaidi duniani.
Kwa miaka ya hivi karibuni pia kumekuwa na tetesi za mara kwa mara kuhusu uwezekano wa wawili hao kuungana tena katika klabu moja.
Inadaiwa Haaland aliwahi kumshawishi Bellingham kujiunga na Manchester City wakati vilabu vikubwa vya Ulaya vilipokuwa vikimuwania.
Baadaye, Bellingham naye ameripotiwa kumshawishi Haaland kuhamia Real Madrid kwa kumsimulia maisha mazuri ya Santiago Bernabeu na namna ambavyo angeendana na mazingira ya soka la Hispania.
Mojawapo ya kumbukumbu kubwa kati yao ilitokea Februari 2025, wakati Bellingham alipofunga bao la ushindi dakika za mwisho dhidi ya Manchester City katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ingawa Haaland alifunga mabao yote mawili ya City, Real Madrid ilishinda 3-2 baada ya Bellingham kufunga bao la ushindi katika dakika ya 92.
Sasa, marafiki hao wa karibu wataweka pembeni urafiki wao kwa dakika 90 watakapokutana uso kwa uso katika robo fainali ya Kombe la Dunia, kila mmoja akipigania nafasi ya kuipeleka nchi yake hatua ya nusu fainali.