Dah! Sir Alex… Safari ya maumivu, uvumilivu na upendo usioyumba
Muktasari:
- Hata hivyo, kipindi tangu astaafu 2013 kimemweka meneja huyo mashuhuri katika majaribu ambayo hata soka halikuwahi kumletea.
MANCHESTER, ENGLAND: KWA mashabiki wa Manchester United, Sir Alex Ferguson daima amekuwa mfano wa nguvu na ustahimilivu.
Hata hivyo, kipindi tangu astaafu 2013 kimemweka meneja huyo mashuhuri katika majaribu ambayo hata soka halikuwahi kumletea.
Hatua kubwa ya kwanza ilitokea Mei 2018, alipokumbwa ghafla na damu kuvuja kwenye ubongo, iliyohitaji upasuaji wa dharura ili kuokoa maisha yake. Akiwa hospitalini, Sir Alex alijikuta akijiuliza, “nimebakiza siku ngapi za kuishi?”
Kwa kuzingatia hali aliyokuwa nayo, hofu yake ilikuwa ya kueleweka. Madaktari waliamini kuwa nafasi yake ya kuishi alipofikishwa Hospitali ya Salford Royal ilikuwa asilimia 20 tu.
“Kulikuwa na visa vitano vya damu kuvuja kwenye ubongo siku hiyo,” amesema Ferguson, aliyekuwa na umri wa miaka 79 wakati huo, akisimulia kwenye filamu ya maandishi ya mwaka 2021 ‘Sir Alex Ferguson: Never Give In’.
“Watu watatu walifariki. Wawili waliinuka tena. Unatambua jinsi ulivyokuwa na bahati.
“Ilikuwa siku nzuri sana, nakumbuka hilo. Nilijiuliza ni siku ngapi za jua ningeziona tena. Hilo lilikuwa gumu kulikubali.”
Mwanzoni mwa safari yake ya kupona, bingwa huyo wa mataji 13 ya Ligi Kuu England aliogopa kuwa huenda akapoteza kumbukumbu zake kabisa baada ya hali yake kuzorota na kumfanya ashindwe kuzungumza vizuri.
“Nilikuwa najitahidi kulisema neno lakini halikutoka,” alieleza. “Daktari mmoja aliingia na nilikuwa nalia kwa sababu nilijisikia sina msaada.”
Akikumbuka wakati alipoanguka nyumbani, Ferguson alikiri kuwa hisia za upweke na hofu ya kifo zilimjia.
“Nyakati ambazo uko peke yako, hofu na upweke huanza kuingia akilini,” amesema. “Hutaki kufa. Hapo ndipo nilipokuwa. Mawazo hayo yalipita akilini mwangu mara nyingi.”
Ingawa Ferguson hatimaye alipona kabisa, miaka iliyofuata ilileta mabadiliko makubwa katika maisha yake binafsi. Mwishoni mwa 2023, Sir Alex alivunjika moyo kufuatia kifo cha mke wake wa miaka 57, Lady Cathy, ambaye mara nyingi alimuelezea kama nguzo ya maisha yake.
Pia amewahi kusema kuwa Cathy ndiye mtu pekee ambaye hakuwahi kumjibu kwa jeuri, kauli ya kushangaza kutoka kwa mtu aliyefahamika kwa kutoa “hairdryer treatment” kali kwa wachezaji waliokuwa hawafanyi vizuri.
Wenza hao walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 1964 walipokuwa wakifanya kazi katika kiwanda cha mashine za kuandikia, na wakafunga ndoa miaka miwili baadaye. Cathy alikuwa na ushawishi mkubwa katika maisha ya Ferguson, akimpa utulivu na msaada, pamoja na kuathiri maamuzi muhimu, ikiwamo kumshawishi kubadilisha uamuzi wake wa kustaafu mwaka 2002.
Baada ya kifo chake, Sir Alex alikiri kuwa alipata shida hata kutoka nje ya nyumba. Akiwa amezama kwenye huzuni, aliamua kusafiri ili kujisahaulisha, akitembelea maeneo kama Saudi Arabia, Hong Kong na Bahrain.
Aliporudi nyumbani, alijiunga na kikundi cha msaada kwa watu wenye changamoto za kumbukumbu (dementia), na baadaye akaamua kuuza nyumba yake ya thamani ya Pauni 3.25 milioni huko Cheshire, aliyokuwa akiishi na Cathy tangu mwaka 2010. Sasa Sir Alex anaishi katika kijiji cha Goostrey karibu na Knutsford, jirani na mwanaye Darren.
Tangu astaafu ukocha, Man United imeendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya Ferguson. Gwiji huyo wa Uskochi bado anahudhuria mechi mara kwa mara akiwa kwenye jukwaa la wakurugenzi.
Hata hivyo, nafasi yake ya kulipwa kama balozi wa klabu ilisitishwa mwaka jana kama sehemu ya hatua za kupunguza gharama zilizoanzishwa na mmiliki Sir Jim Ratcliffe. Mwenyekiti wa INEOS, ambaye alinunua asilimia 25 ya hisa za klabu hiyo Februari 2024, amesimamia mamia ya wafanyakazi kufutwa kazi Man United.
Inaripotiwa kuwa Ferguson alikuwa akilipwa Pauni 2 milioni kwa mwaka, na ingawa alielezwa kuwa “ulikuwa mkunjo kidogo” na Ratcliffe alipoelezwa kuwa nafasi hiyo ingeisha, hatimaye alikubali kwa heshima.
“Ninamheshimu sana Alex,” amesema Sir Jim.
“Niliketi chini na Alex, sisi wawili tu. Nikamwambia, ‘Tazama, klabu haipo katika hali unayodhani. Inatumia zaidi ya inachopata, na tuko hatarini kifedha. Kwa kweli hatuwezi kumudu kuendelea kukulipa Pauni 2 milioni kwa mwaka.’
“Nikamwambia, ‘Nitakuachia utafakari hilo.’ Ilikuwa mazungumzo ya watu wazima. Labda alikuwa na mkunjo kidogo mwanzoni, lakini alielewa. Alirudi baada ya siku tatu, baada ya kuzungumza na mwanaye, na akasema, ‘Sawa, nitaachana nayo. Ni uamuzi wangu.’”
Aliendelea kusema: “Nadhani hilo linaonyesha tabia njema ya Alex kwa sababu aliitanguliza klabu kuliko maslahi yake binafsi.”