Cole akaribishwa Italia kwa kipigo
Muktasari:
- Kocha huyo mpya ameshuhudia timu yake ikipoteza kwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Mantova, ambapo kipigo hicho kimepunguza matumaini ya klabu hiyo kupata nafasi ya kucheza mechi za mtoano msimu huu. Msimu uliopita ilimaliza nafasi ya saba kati ya timu 20 za ligi hiyo.
CESENA, ITALIA: BEKI wa zamani wa kushoto wa Chelsea na Arsenal, Ashley Cole ameanza vibaya katika kibarua chake cha kwanza kama kocha mkuu wa timu ya ya Cesena inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Italia (Serie B).
Kocha huyo mpya ameshuhudia timu yake ikipoteza kwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Mantova, ambapo kipigo hicho kimepunguza matumaini ya klabu hiyo kupata nafasi ya kucheza mechi za mtoano msimu huu. Msimu uliopita ilimaliza nafasi ya saba kati ya timu 20 za ligi hiyo.
Cesena inalenga kupanda Serie A kwa mara ya kwanza tangu ilipoanzishwa upya mwaka 2018. Timu hiyo ilianzishwa 1940 ikifahamika kama AC Cesena kabla ya miaka minane iliyopita kubadili jina na kuanza kuitwa Cesena FC.
Baada ya kuthibitishwa kuwa kocha mkuu wikiendi iliyopita, Cole aliongoza timu yake kwa mara ya kwanza walipoifuata Mantova. Hata hivyo, walijikuta nyuma mapema dakika ya sita kufuatia bao la kujifunga la Giovanni Zaro.
Andrea Meroni na Leonardo Mancuso walifunga mabao mawili ya kipindi cha pili na kuipa Mantova ushindi wa pointi tatu. Mantova walikuwa nafasi ya 15 kabla ya mechi hiyo, lakini walitoa pigo kwa ndoto za Cesena za kupanda daraja.
Matokeo hayo yana maana kuwa Cesena inaweza kushuka nje ya nafasi za mtoano. Timu zinazomaliza nafasi ya tano hadi ya nane huingia hatua ya awali ya mtoano, huku washindi wakijiunga na waliomaliza nafasi ya tatu na nne katika nusu fainali.
Pia, kipigo hicho kimeondoa kabisa matumaini madogo ya Cesena kupanda daraja moja kwa moja msimu huu.
Kwa sasa wako nyuma kwa pointi 24 dhidi ya timu mbili za juu huku zikiwa zimebaki mechi saba pekee.
Cole atakuwa na matumaini ya kurejea kwa ushindi katika mechi yake ya kwanza ya nyumbani dhidi ya Catanzaro, leo, Jumamosi. Cesena haijacheza Serie A tangu 2015, kabla ya kuvunjwa miaka mitatu baadaye na kisha kuanzishwa upya.
Kwa upande wa Cole, hiyo ndiyo kazi yake ya kwanza kama kocha mkuu baada ya kuwa msaidizi wa Lee Carsley katika timu ya England chini ya umri wa miaka 21.
Aliwahi pia kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Carsley alipokuwa kocha wa muda wa timu ya taifa ya wakubwa ya England. Pia aliwahi kuwa kocha msaidizi katika timu za Everton, Chelsea na Birmingham City. Akiwa mchezaji, Cole alicheza mechi 384 za Ligi Kuu England akiwa na Chelsea na Arsenal. Pia alishinda mataji 16 makubwa yakiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya na mataji matatu ya Ligi Kuu.