Chuma Casemiro kinaondoka, watu wa kazi wagombea buti zake!
Muktasari:
- Man United walikuwa na chaguo la kuongeza mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi, lakini hawakuwa na nia ya kulitumia.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa boli, Casemiro ataondoka Manchester United mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.
Man United walikuwa na chaguo la kuongeza mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi, lakini hawakuwa na nia ya kulitumia.
Casemiro alitaka kutangaza wazi kuondoka kwake Man United jambo ambalo klabu ililikubali, lakini vyanzo vinasisitiza uamuzi wa kutomwongezea mkataba ulikuwa umefanywa muda mrefu kabla ya tangazo hilo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alitaka kuweka wazi mustakabali wake na kuepusha uvumi wowote angeweza kubaki Man United kwa mwaka mwingine.
Amesema: “Nitabeba Manchester United moyoni mwangu maisha yangu yote. Kuanzia siku ya kwanza nilipoingia kwenye uwanja huu mzuri, nilihisi shauku ya Old Trafford na upendo ninaoshiriki sasa na mashabiki wetu kwa klabu hii ya kipekee.
"Sio wakati wa kusema kwaheri; bado kuna kumbukumbu nyingi za kuunda katika miezi minne ijayo. Bado tuna mengi ya kupigania pamoja, umakini wangu wote, kama kawaida, utabaki katika kutoa kila kitu kusaidia klabu yetu kufanikiwa.”
Casemiro, ambaye alikuwa mmoja wa usajili wa kwanza katika enzi isiyo na mafanikio ya Kocha Erik ten Hag, anakiri sasa ni wakati wa kuendelea na hatua mpya maishani.
Aliandika kwenye Instagram: “Kujua wakati hatua zinapofikia mwisho. Kujua wakati wa kusema kwaheri unapohisi kuwa utakumbukwa na kuheshimiwa milele.
"Miezi minne ya kutoa kila kitu kwa beji hii na kwa lengo letu. Heshima na upendo wa milele kwa Manchester United na mashabiki wake wa ajabu. Daima Shetani Mwekundu.”
Kuondoka kwa Casemiro kutafungua nafasi ya kifedha kwa Man United kufanya usajili mkubwa wa kiungo wa kati.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil ni mmoja wa wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi klabuni, akipata takribani Pauni 300,000 kwa wiki.
Man United wanafuatilia wachezaji wa England, Elliot Anderson, Adam Wharton na Alex Scott, pamoja na kiungo wa Brighton, Carlos Baleba.
Lengo kuu la klabu dirisha lijalo la usajili la majira ya kiungo ni kusajili kiungo Namba 6.
Casemiro, ambaye atatimiza miaka 34 mwezi ujao, alijiunga na Man United kutoka Real Madrid kwa dau la Pauni 70 milioni, Agosti 2022.
Baada ya msimu wake wa kwanza wenye ushawishi mkubwa ambapo alifunga bao la ushindi katika fainali ya Kombe la Ligi, Casemiro alipitia msimu wa pili wa kusahaulika na aliachwa nje ya kikosi cha fainali ya Kombe la FA 2024 chini ya Kocha Ten Hag.
Mashabiki wa Old Trafford walikuwa wa haraka kumshukuru mchezaji huyo mwenye mechi 82 za timu ya taifa ya Brazil baada ya habari za kuondoka kwake kuthibitishwa.
Kuondoka kwa Casemiro ni mojawapo ya habari zisizoshangaza kabisa kutoka Man United msimu huu. Alikuwa ataachwa bila shaka. Ingeshangaza sana kama angebaki.
Ni mmoja wa wachezaji wanaolipwa zaidi klabuni, karibu Pauni 350,000 kwa wiki, na anatimiza miaka 34 mwezi ujao. Msimu wake bora ulikuwa wa kwanza, hivyo haingekuwa na mantiki kwa United kumbakiza kwa mwaka wa tano.
Kiwango chake kwa mwaka mmoja uliopita kilikuwa cha wastani, kikijikita zaidi kwenye michuano ya Ulaya msimu uliopita.
Hata hivyo, alikuwa shujaa katika kurejea kwa ajabu dhidi ya Lyon kwenye robo fainali ya Europa League na Man United walitoka nyuma ya mabao 4-2 na kushinda 5-4.
Huyu shabiki amesema: "Kwa haki yake, msimu huu hakuwa mzigo kama wengine walivyotarajia, hasa kutokana na kasi ya Ligi Kuu."
Katika kipindi ambacho kulikuwa na mechi moja kwa wiki na Manuel Ugarte hakuwa wa kuaminika, Casemiro alijitahidi na kufanya vizuri kiasi.
Kwa mshangao, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi katika dabi ya Manchester wiki iliyopita, ilhali kulikuwa na wachezaji sita au saba waliocheza vizuri zaidi yake. Lakini kwa mtazamo wake, ali onyesha klabu vinavyoweza kumtaka kwamba bado ana uwezo.
Hatimaye, kumsajili kiungo aliyezeeka kutoka Real Madrid kwa Pauni 60 milioni (ikiongezeka hadi 70) haikuwa uamuzi mzuri. Hiyo ni kabla ya gharama ya mishahara ya Pauni 73 milioni kwa miaka minne. Man United ililazimika kumsajili Casemiro baada ya kushindwa kumnasa Frenkie de Jong kutoka Barcelona.
Casemiro alikuwa wa kipekee msimu wa kwanza, mgombea halali wa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Man United na alifunga bao la ushindi kwenye fainali ya Kombe la Ligi. Erik ten Hag alimwita “saruji kati ya mawe” kwa sababu alisawazisha kiungo ambacho kilihitaji sana mchezaji wa ulinzi.
Lakini mambo yalianza kuharibika msimu wa pili alipocheza katika kiungo kisichoendana na Mason Mount.
Jaribio hilo lilidumu mechi mbili tu kabla ya Casemiro kuumia na kushindwa kupata mwendelezo. Kwa kujitolea, alicheza mara nyingi kama beki wa kati wakati wa mgogoro wa majeruhi, jambo lililomdhuru zaidi.
Maarufu zaidi ni mechi dhidi ya Crystal Palace na Man United ilipigwa 4-0 na Casemiro alipitwa kirahisi na Michael Olise kwa bao la kwanza. Kujitolea huko kulimgharimu nafasi ya kuanza fainali ya Kombe la FA.
Ten Hag aliamua kuanza na Sofyan Amrabat na baadaye ikabainika Casemiro hakuwa hata benchi kutokana na jeraha fulani. Ilionekana kama pazia la mwisho, lakini alibaki misimu miwili zaidi kwa sababu hakuna aliyekuwa tayari kulipa mshahara wa karibu Pauni 350,000 kwa wiki kwa mchezaji aliyekuwa anapoteza kiwango. Man United ilishindwa kumpata mnunuzi katika dirisha la usajili la majira ya baridi mwaka jana.
Baada ya kipigo dhidi ya Newcastle United, Desemba 2024, Casemiro hakucheza kwa mwezi mzima. Man United ilikuwa wakitumaini tu mnunuzi, lakini nafasi zilikuwa karibu sifuri kabisa. Sio vizuri kuwa na mchezaji wa hadhi hiyo kwenye orodha ya mishahara kwa miezi 18 zaidi.
Hata hivyo, Casemiro ameheshimu mipaka ya uwezo wake na kuelewa kuna mambo hawezi tena kuyafanya. Michael Carrick hivi karibuni alimrudisha kikosini na kumweka benchi Ugarte katika ushindi wa dabi wa mabao 2-0, ambapo Casemiro alicheza kwa utulivu wa kushangaza.
Hatimaye, anaweza kukumbukwa kama usajili wa gharama kubwa uliokosewa, lakini hiyo ni kali kupita kiasi.
Alichangia mojawapo ya misimu miwili iliyofanikiwa baada ya Ferguson na kushinda vikombe viwili. Lakini mazingira ya mkataba wake hayakuonyesha uongozi wa klabu katika mwanga mzuri. Kama Jason Wilcox angeidhinisha kuongezewa mkataba, naye angepaswa kuwa wa kwanza kuondoka.
Mmoja aliandika kwenye X: “Mtaalamu wa kweli aliyevaa beji kwa fahari isiyo na kifani. Inasikitisha hatukumchukua akiwa na miaka ya kati ya 20, kwa sababu shauku na uongozi wake ndivyo klabu hii inajengwa juu yake. Asante kwa kila kitu.”
Mwingine amesema: “Asante kwa kila kitu, Case! Tunakutakia kila la heri mbele yako, rafiki.”
Na mwingine: “Red wa kweli. Asante kwa kila kitu, Uncle Cade. Tunakupenda.”
Mmoja akaandika: “Hakuna kinachodumu milele, kwaheri Casemiro.”
Mwingine akaongeza: “Asante, Case!”
Wanne kuwania buti zake
Man United wameandaa orodha ya wachezaji wanne wanaoweza kumrithi Casemiro anayetarajiwa kuondoka hivi karibuni. Kiungo huyo, aliyekuwa mmoja wa usajili wa kwanza katika enzi isiyofanikiwa ya Erik ten Hag pale Old Trafford, ataondoka klabuni mwishoni mwa msimu huu. Ripoti zinafichua viongozi wa klabu klabu tayari wana majina manne waliyochagua kumrithi Mbrazili huyo anayeondoka. Kwa sasa, wanafuatilia kwa karibu nyota, Elliot Anderson wa Nottingham Forest, Adam Wharton wa Crystal Palace, Alex Scott wa Bournemouth na Carlos Baleba wa Brighton.
Baleba, mwenye umri wa miaka 22, alikuwa lengo la Man United kwenye usajili wa dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana. Jaribio la kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon lilifikiriwa, lakini linaonekana kutotimia kutokana na nafasi ya ukocha kuwa wazi katika klabu ya Old Trafford.
MAN UNITED ILIVYOKUWA IKIMLIPA CASEMORO MISHAHARA YAKE
-Kwa Mwaka: Pauni 18,250,000
-Kwa Mwezi: Pauni 1,520,000
-Kwa Wiki: Pauni 350,000
-Kwa Siku: Pauni 50,000
-Kwa Saa: Pauni 2,089
-Kwa Dakika: Pauni 34.82
-Kwa Sekunde: Pauni 0.58