Christopher Nkunku aingia anga za Man United

Muktasari:
- Mabosi wa Chelsea wapo tayari kumuuza Nkunku baada ya staa huyo kuwasilisha ombi la kutaka kuondoka ili kujiunga na timu itakayompa nafasi zaidi ya kucheza.
CHELSEA imeiambia Manchester United kwamba italazimika kulipa pauni 35 milioni iwapo inataka kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Christopher Nkunku, 27, katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Mabosi wa Chelsea wapo tayari kumuuza Nkunku baada ya staa huyo kuwasilisha ombi la kutaka kuondoka ili kujiunga na timu itakayompa nafasi zaidi ya kucheza.
Man United inapambana kuhakikisha inaboresha safu yake ya ushambuliaji katika dirisha hili na imemwongeza Nkunku katika orodha yao kama mbadala ikiwa itashindwa kufanikisha madili ya mastaa iliowaweka vipaumbele ambao ni Viktor Gyokeres na Bryan Mbeumo.
Mkataba wa Nkunku unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Msimu uliopita alicheza mechi nne za michuano yote na kufunga bao moja.
Nkunku sasa anaonekana kutokuwa tena muhimu katika mipango ya Chelsea, kufuatia usajili wa Joao Pedro na Liam Delap waliogharimu jumla ya pauni 90 milioni katika dirisha hili la uhamisho la majira ya kiangazi.
Chelsea pia imethibitisha usajili wa Jamie Gittens kutoka Borussia Dortmund kwa dau la pauni 52 milioni, ikiendeleza mtindo wao wa matumizi makubwa.
Hata hivyo, baada ya kutozwa faini kubwa ya pauni 78.5 milioni na UEFA kwa kuvunja kanuni za matumizi ya fedha, Chelsea sasa inalazimika kuuza baadhi ya wachezaji.
Nkunku, yupo kwenye rada ya Manchester United, ingawa klabu hiyo pia inamwangalia mshambuliaji wa Aston Villa, Ollie Watkins.
United wanapanga kumuuza kinda wao Alejandro Garnacho, ambaye hapo awali alivutia Chelsea, lakini vikwazo vya kifedha na masharti ya UEFA vinaweza kuathiri mipango hiyo, kwa mujibu wa gazeti la Express.
Hali hii ingefungua uwezekano wa dili la kubadilishana wachezaji, lakini Chelsea huenda wakalazimika kuzingatia uuzaji wa moja kwa moja ili kupunguza ukubwa wa kikosi chao.
Wakiwa na washambuliaji kama Nicolas Jackson, ambaye rekodi yake ya kinidhamu imekuwa tatizo, Chelsea wanakabiliwa na maamuzi mengi kuelekea msimu mpya.
Usajili wa nyota wa Brazil, Pedro, ambaye anaweza kucheza kama mshambuliaji wa kati au pembeni, umeongeza mashaka juu ya mustakabali wa Nkunku katika kikosi cha Chelsea.
Ingawa huenda Nkunku si chaguo la kwanza kwa Manchester United, anaweza kuwa mbadala wa gharama nafuu, hasa ikizingatiwa kuwa United wanamhitaji Bryan Mbeumo, huku tayari wakiwa wameshamchukua Matheus Cunha kutoka Wolves.
Ethan Nwaneri
WAWAKILISHI wa Chelsea wanamfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Arsenal na timu ya taifa ya England chini ya miaka 21, Ethan Nwaneri, 18, wakati huu ambapo anaendelea kufanya mazungumzo ya mkataba mpya na Arsenal.
Inaelezwa Chelsea inataka kuingilia kati dili hilo kwa kuweka mkwanja wa kutosha ambao wanaamini utamshawishi ajiunge nao. Arsenal inasemekana kumwania Noni Madueke.
Son Heung-min
MSHAMBULIAJI wa Tottenham na timu ya tafa ya Korea Kusini, Son Heung-min, 32, amekataa ofa ya Los Angeles FC waliyoiwasilisha ili kumsajili katika dirisha hili.
Son anadaiwa kuwa tayari kuondoka lakini bado anaamini anaweza kucheza soka la kiushindani barani Ulaya na ikishindikana kusalia Ulaya anataka kusaini timu ambayo itampa pesa maradufu ya zile ambazo anazipata kwa sasa.
Chemsdine Talbi
SUNDERLAND ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na Club Brugge kuhusu kumsajili winga mwenye umri wa miaka 20, Chemsdine Talbi ambaye amezaliwa Ubelgiji lakini amechagua kuiwakilisha Morocco.
Mkataba wa sasa wa Talbi unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu uliopita alionyesha kiwango bora ambapo alicheza mechi 44 za michuano yote na kufunga mabao saba.
Josh Sargent
BURNLEY na Leeds zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Norwich na Marekani, Josh Sargent, 25, ili kumsajili katika dirisha hili.
Inaelezwa Norwich ipo tayari kumuuza lakini inahitaji walau pauni 16 milioni kama ada ya uhamisho. Mkataba wake unamalizika mwaka 2028.
Hakan Calhanoglu
INTER Milan imekataa ofa ya euro 17 milioni kutoka kwa Galatasaray ili kumuuza kiungo wake wa kimataifa wa Uturuki, Hakan Calhanoglu, katika dirisha hili la uhamisho la majira ya kiangazi.
Inaelezwa Inter ipo tayari kumuuza kiungo huyo lakini inaamini thamani yake ni zaidi ya Euro 34 milioni ambayo ni kubwa kuliko ofa ambayo Galatasaray imeiwasilisha.
Ciro Immobile
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Italia anayeichezea Besiktas ya Uturuki, Ciro Immobile, mwenye miaka 35, anatarajia kuvunja mkataba wake na timu hiyo na kujiunga na Bologna bila ada ya uhamisho.
Katika msimu uliopita Ciro alicheza mechi 41 za michuano yote na kufunga mabao 19. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani.
Andreas Christensen
AC Milan ni kati ya timu zilizojiingiza katika vita ya kuiwania saini ya beki wa Barcelona na timu ya taifa ya Denmark, Andreas Christensen, 29, ambaye amepewa ruhusa ya kuondoka katika dirisha hili ikiwa atapata timu itakayokuwa tayari kumsajili. Mabosi wa Barca wanataka kumwondoa Andreas kwa sababu tayari ina mabeki wa kati watano.