Chelsea yafikiria kumrudisha Hazard

Thursday July 22 2021
hazard pic

LONDON, ENGLAND. MATAJIRI wa London, Chelsea wanatafakari wazo la kumrudisha aliyekuwa mshambuliaji wao,  Eden Hazard kutoka Real Madrid ya Hispania  msimu huu wa joto, kulingana na ripoti.

Nahodha huyo wa timu ya taifa la Ubelgiji amekuwa na wakati mgumu tangu ajiunge na miamba hiyo ya Hispania akitokea Chelsea kwa uhamisho wa Pauni 88milioni, nyota huyo mwenye umri wa miaka 30, ameichezea timu hiyo michezo 21 tu msimu uliopita.

Kiujumla,Hazard ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara ameifungia Real Madrid mabao matano kwenye mashindano yote.

Kwa mujibu wa chombo kimoja cha habari huko Hispania, imeripotiwa kwamba, Chelsea wanatafakari juu ya uwezekano huo na kwa upande wa Real Madrid imeelezwa kwamba wapo tayari kumwachia Mbelgiji huyo kwa Pauni 51milioni.

Real Madrid wapo tayari kumwachia Hazard ili kujichanga kwa ajili ya kuinasa saini ya mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Erling Haaland anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 170milioni, Chelsea nao wapo kwenye vita ya kumuwania Mnorway huyo.

Msimu uliopita, Hazard aliwakwaza mashabiki wa Real Madrid kutokana na kitendo cha  kuonekana akifurahi na wachezaji wa Chelsea, Kurt Zouma na Edouard Mendy mara baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa  kumalizika huku chama lake likifungashiwa virago.

Advertisement

Licha ya kuomba radhi kwa tukio hilo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, mashabiki walimtafsiri Hazard kuwa ni mwili wake tu ambao upo Madrid lakini moyo wake wote upo Stamford Bridge.Advertisement