Chelsea Yachekelea Kane kuwabeba

Muktasari:
- Nahodha huyo wa England, Kane alipata nafasi muhimu kabisa ya kufunga ili kuipa sare Bayern kwenye mechi dhidi ya Benfica katika mchezo uliofanyika uwanja wa Bank of America.
LOS ANGELES, MAREKANI: MASHABIKI wa Chelsea wanaamini kwamba timu yao imepata fursa nzuri ya kufika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani kwa msaada wa makosa ya Harry Kane kukosa bao la wazi la kuifungia Bayern Munich.
Nahodha huyo wa England, Kane alipata nafasi muhimu kabisa ya kufunga ili kuipa sare Bayern kwenye mechi dhidi ya Benfica katika mchezo uliofanyika uwanja wa Bank of America.
Kwa hivyo, Bayern ikapoteza mechi hiyo kwa bao 1-0 na hivyo kutoa nafasi ya Chelsea kuwa na njia isiyokuwa na vikwazo vingi katika kuelekea fainali ya michuano hiyo.
Ushindi wa Benfica umeifanya kuwa kinara wa Kundi C, wakati Kane na chama lake la Bayern wakiishika kushika namba mbili. Kwa maana hiyo, Chelsea sasa itacheza na Benfica kwenye hatua ya 16 bora, wakati Bayern itakuwa na kasheshe la kuwakabili Flamengo.
Chelsea imemaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D, huku Wabrazili, Flamengo wakiwa vinara.
Na mashabiki wa Chelsea sasa wanaona kama hiyo ni fursa bora kwao kufika fainali.
Shabiki mmoja aliandika mtandaoni: “Jinsi gani njia yetu ilivyotengenezwa hadi fainali.”
Mwingine aliongeza: “Kimkakati kabisa Chelsea tumemaliza namba mbili, nimependa.”
Shabiki wa tatu aliandika: “Njia tamu kwa Chelsea.
Na shabiki wa nne alisema: “Njia yetu ya kufika nusu fainali, kwa sasa Benfica kisha watakuja Palmeiras au Botafogo. Tumewakwepa PSG na Bayern. Na tunaye Delap na mastaa kibao.”
Mwingine alisema: “Asante Flamengo kwa kutufunga.”
Chelsea kama itafanikiwa kupenya kwa Benfica itakwenda kukabiliana na ama Palmeiras au Botafogo. Na kama itapenya, itakuwa na kibarua cha ama kuwakabili mabingwa wa Ulaya, PSG au Inter Miami ya supastaa wa boli, Lionel Messi.