Chelsea: Conor siyo mbaguzi wa rangi

LONDON, ENGLAND. BAADA ya kusambaa kwa video iliyokuwa inamuonyesha mchezaji wa Chelsea, Conor Gallagher akikataa kumpa mkono mtoto mmoja mwenye rangi nyeusi wakati wa kuingia uwanjani katika mechi dhidi ya Burnley, Chelsea imesema kilichofanywa haukuwa  ubaguzi wa rangi.

Tukio hilo lilitokea wikiendi iliyopita wakati wachezaji wamejipanga kwa ajili ya kuingia uwanjani mtoto mmoja mwenye asili ya Kiafrika alimpa mkono Conor, lakini staa huyo aliukataa na badala yake akamshika tu kichwani.

Watu wengi mitandaoni walimshambulia staa huyo kwa maneno  wakimwambia kwamba amefanya kitendo hicho wakikihusisha na ubaguzi wa rangi.

Katika taarifa iliyotolewa leo, Chelsea imepinga na kusema maneno ambayo mchezaji wao anashambuliwa nayo kwamba ni mbaguzi wa rangi hayakubaliki.

"Tunajivua kuwa timu inayojumuisha watu wa aina zote kutoka tamaduni zote," imesema taarifa ya klabu hiyo.

Katika mechi hiyo Chelsea iliambuliwa sare ya mabao mabao 2-2 na kuendelea kujiweka kwenye mazingira magumu ya kufuzu michuano ya Ulaya mwakani.