Chelle: Tupo tayari kuikabili DR Congo
Muktasari:
- Nigeria itamenyana na kikosi cha Sebastian Desabre katika mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Prince Héritier Moulay El Hassan, Rabat, saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Nigeria maarufu Super Eagles, Éric Chelle, amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mechi ya fainali ya mchujo ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya DR Congo, leo Jumapili, Novemba 16, 2025.
Nigeria itamenyana na kikosi cha Sebastian Desabre katika mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Prince Héritier Moulay El Hassan, Rabat, saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Chelle amesema mechi ya leo, ni nafasi nyingine kwa timu yake kupata nafasi ya kuendelea kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, baada ya kukosa nafasi hiyo katika hatua ya makundi.
Amesema ameshakamilisha maandalizi yote na kila mchezji wake yupo tayari kwa mpambano huo, ambao ameutabiri kuwa na upinzani mkubwa kutokana na kila upande kuhitaji kusonga mbele.
“Tumejipanga vizuri kuikabili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tunajua nini cha kufanya ili kufikia lengo tulilojiwekea, japo wapinzani wetu wana uwezo mkubwa wa kukabiliana na timu yoyote duniani kwa sasa.
“Nimejitahidi kufanya kila linalowezekana katika uwanja wa mazoezi, kila mchezaji wangu ameonyesha kuwa tayari kupambana, hivyo kazi yetu itaonekana ndani ya dakika 90, ili kufanikisha mpango wa kuendelea kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026,” amesema Chelle.
Ushindi katika mechi hiyo unaosubiriwa kwa hamu kubwa utaifanya timu itakayoshinda kushiriki katika mchuano wa mtoano wa mabara mbalimbali (Intercontinental Playoffs) Machi 2026.
Mashindano hayo madogo yatafanyika katika miji miwili ya Guadalajara na Monterrey nchini Mexico.
Timu nyingine kutoka nje ya Afrika ambazo zinatarajiwa kushiriki Intercontinental Playoffs, zinatoka mabara tofauti.
Kutoka Amerika Kusini, Bolivia imetambulika kama mmoja wa washiriki. Kutoka Oceania, New Caledonia itachukua nafasi yao kwenye michuano hiyo. Kutoka Asia (AFC), kuna nafasi moja ya mchujo ambayo itatolewa kwa timu itakayofika hatua ya mwisho ya mchujo wa bara hilo.
Aidha, kutoka CONCACAF (Amerika Kaskazini, Amerika ya Kati na Karibiani), ripoti zinaonyesha kuwa timu mbili zitaruhusiwa kushiriki kwenye playoffs ya intercontinental.
Hii inatoa fursa ya kipekee kwa timu zinazoshiriki kufuzu moja kwa moja kwa Kombe la Dunia, ikiwa haziwezi kupata tiketi kupitia mchujo wa moja kwa moja wa bara lao.