Cheki balaa la mizuka ya kocha Simeone

Muktasari:
Huduma na rekodi zake kwenye kikosi cha Los Rojiblancos sio ya mchezo mchezo hata kidogo, lakini Simeone pia anarekodi zingine matata kabisa za kuondolewa uwanjani na kufungiwa mechi zaidi ya 20.
MZUKA wa kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone umekuwa ukiwapagawisha wachezaji wake uwanjani, lakini una madhara makubwa kwake kutokana na kuingia kwenye migogoro na waamuzi.
Huduma na rekodi zake kwenye kikosi cha Los Rojiblancos sio ya mchezo mchezo hata kidogo, lakini Simeone pia anarekodi zingine matata kabisa za kuondolewa uwanjani na kufungiwa mechi zaidi ya 20.
Rekodi zinaonyesha kwamba, tangu Simeone ameingia kwenye kazi ya ukocha, amepewa adhabu ya kukaa jukwaani mara sita huku akifungiwa mechi 20 kutokana na kukiuka kanuni na kuwaingilia waamuzi.
Simeone anafahamika kwa kuwa na mzuka anaposimama kwenye mstari kuwapa maelekezo wachezaji wake, pia staili yake ya kushangilia lakini inapokuja mwamuzi kutoa maamuzi tofauti mzuka wake hupanda zaidi.
Kwa mara ya kwanza alitolewa nje na mwamuzi Bjorn Kuipers kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kisha akakutana na adhabu kama hiyo miezi mitatu baadaye kwenye fainali ya Supercopa de Espana kwa mwamuzi David Fernandez Borbalan.
Pia, alifungiwa mechi nane kutokana na kumvamia mwamuzi wa akiba kwa maneno makali huku akimvuta kwa nyuma.
Bahati mbaya kwa Semeone, amekuwa akikutana na rungu la mwamuzi Borbalan mara kwa mara, ambapo alimtoa nje kocha huyo mara mbili ndani ya msimu mmoja.
Katika msimu wa 2014/2015, Muagentina huyo alitolewa nje ya uwanja kwa vitendo vyake hivyo kisha akafungiwa mechi moja.
Msimu uliofuata, Simeone alitolewa nje na mwamuzi Antonio Mateu Lahoz baada ya kupiga mpira jukwaani wakati akijaribu kuzima mashambulizi ya Malaga kwenye dakika za lala salama.
Bila kupoteza muda Lahoz alimtoa Simeone nje na baadaye alikutana na adhabu zaidi ya kufungiwa mechi tatu, hata hivyo huwa hajali.
Msimu huu kwenye robo fainali ya Copa del Rey, mwamuzi Juan Martinez Munuera alimtoa nje El Cholokisha kufungiwa mechi tatu alimsemea mbovu mwamuzi huyo wakati akitoka nje ya uwanja.
Kivumbi cha maana ni cha hivi karibuni, ambapo El Cholo amekuwa akitoa maelekezo akiwa jukwaani kutokana na kufungiwa na UEFA kutokana na kuwazingua waamuzi.
Alitolewa nje kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza dhidi ya Arsenal pale Emirates kisha kukumbana na adhabu ya kufungiwa mechi nne. Katika mchezo wa kwanza, timu hizo zilikwenda sare ya bao 1-1, lakini mchezo wa pili ndio ulikuwa na mzuka mwingi kwa El Cholo.
Akiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Wanda Metropolitano, El Cholo alikaa eneo la peke yake jukwaani na muda wote alisikika akipiga kelele huku akipandwa mizuka pindi mastaa wake wanapokosa bao.
Bao pekee la straika mtukutu, Diego Costa ndio lilimtia ukichaa El Cholo, ambaye muda wote alikuwa akishangilia kwa staili ya kuzungusha skafu ya Atletico na kuufanya uwanja mzima kurindima kelele.