Celtics yaipa hesabu ngumu Lakers NBA

Muktasari:
- Celtics ilicheza fainali mwaka huo dhidi ya Golden State Warriors na kupoteza katika msimu ambao wengi waliipa nafasi kubwa ya kulichukua taji hilo.
JUMANNE wiki hii, Boston Celtics ya Ukanda wa Mashariki, ilishinda taji la kwanza kwao baada ya 16, huku ikisahihisha makosa ya mwaka 2022 ilipokaribia kulinyakua kabla ya kufungwa kwenye fainali na sasa msala imeuacha kwa Los Angeles Lakers ya mkali LeBros James.
Celtics ilicheza fainali mwaka huo dhidi ya Golden State Warriors na kupoteza katika msimu ambao wengi waliipa nafasi kubwa ya kulichukua taji hilo.
Ni hivi, kabla ya kuifikia na kuipita rekodi ya kubeba mataji mengi iliyokuwa kwa Lakers na kubeba baada ya zaidi ya miaka 10, Celtic ina kazi ya kufanya kuhakikisha hainyang’anywi taji hilo na Lakers ili kuifikia kwa Idadi.
Hadi sasa Celtic ndiyo inaongoza kwa kubeba mara nyingi (18) baada ya kuifunga kwenye fainal Dallas Mavericks na msala upo kwa Lakers msimu ujao.
Kinachoelezwa ni Lakers inajipanga upya baada ya kumtangaza kocha mpya ambaye hajawahi kuinoa timu yoyote kwenye NBA.
JJ Redick kutoka kuwa mchambuzi wa mechi za NBA, hadi kuwa kocha mpya wa Lakers imeshtua wengi na zaidi kuwahi kufanya kipindi maalumu na LeBron inatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kupewa kwake jukumu la kuinoa Lakers msimu ujao.
MATAJI MENGI ZAIDI
Sasa Celtics ndio inakuwa timu yenye mafanikio zaidi kwenye historia ya ligi hii, kwa kutwaa mataji mengi zaidi ambayo ni rekodi mpya, huku timu nyingine zikishindwa angalau kufikisha mataji 10 ukiachana na Lakers inayofuata kwa mataji 17 kwenye timu zilizochukua mataji mengi ya NBA.
Golden State Warriors inafuata kwa kuchukua mataji saba, Chicago Bulls ikichukua mataji sita, San Antonio Spurs (5) huku timu tatu za Philadelphia 76ers, Detroit Pistons na Miami Heat zikitwaa mataji matatu.
BILL RUSSELL AMEACHA REKODI
Wakati Celtics inacheza fainali ya NBA mwaka 2022 na Warriors na kupoteza, siku kadhaa mbele, gwiji wao Bill Russell alifariki dunia (Julai), akiwa na miaka 88 na bila shaka angekuwepo angeshuhudia hatimaye timu yake aliyoichezea muda wote na kushikilia rekodi nyingi ikichukua tena taji hilo.
Russell anabaki kuwa ndiye mchezaji mwenye mataji mengi zaidi ya NBA, akichukua mataji 11 ya NBA akiitumikia Celtics, kama walivyo nyota wengine Sam Jones mwenye mataji 10 na K. C. Jones aliyechukua mataji nane, hao wote wakiwa sehemu ya Celtics ya mafanikio zaidi kiasi cha kuifanya kuwa timu yenye mataji mengi NBA.